RIZIKI TOLEO LA 2/2024

Page 1

RIZIKI TOLEO LA 2/2024 NIKO HAPA! NITUME MIMI
Juni/2024 - Agosti/2024

RIZIKI

S.L.P. 2696, Arusha 0759 544 917

Barua pepe: editor.somabiblia@gmail.com

Kamati ya Riziki:

James Sabuni (mhariri)

Mch. Anza Amen Lema

Mch. Philip Bach-Svendsen

Cathbert Msemo

Mary Bura

Magreth Mushi

Mch. Gervas Meitamei Luhekelo Sanga

Waandishi walioshiriki:

Mch. Gideon Mumo

Mch. Goodluck Elias Msumari

Mch. Oswald Ndelwa

Mch. Rivas Kibona

Layout: Cathbert Msemo

Jalada: www.pixabay.com

ISSN 2683 - 6491

Nakala: 5000

Usambazaji: SOMA BIBLIA

S.L.P. 2696, Arusha

S.L.P. 12772, Dar es Salaam

S.L.P. 1088, Iringa

S.L.P. 6097, Mwanza

S.L.P. 1062, Mbeya

S.L.P. 4231, Dodoma

www.somabiblia.or.tz

Neno la Injili kwa rika zote Tanzania!

Imechapwa na:

Imaging Smart Dar es Salaam

Hawakuwa watu maarufu

Kazi nyingi wanazopewa watu ni kutokana na ujuzi au mahitaji ya kazi yenyewe. Ndiyo maana kuwa na usaili ili mwenye kazi ahakikishe kuwa amepata mtu sahihi wa kufanya kazi yake. Kwa umuhimu wa kazi husika, matangazo yake yanatolewa hadi kwenye radio, runinga, magazeti na hata mitandao ya kijamii. Lengo ni kupata mtu sahihi kwa imani kwamba uzoefu wake, elimu yake na sifa nyinginezo zitaweza kuwa msaada kwa mahitaji ya mwenye hiyo kazi. Swali tunaloweza kujiuliza ni kwa nini wakati Yesu alipochagua wanafunzi wake hakuchagua wasomi na watu wenye ujuzi wa mambo ya dini ili ujuzi wao umsaidie katika huduma yake hapa duniani? Na je, alitumia vigezo gani kuchagua wanafunzi ambao aliwaachia kuhubiri Injili baada ya yeye kurudi mbinguni?

Mada kuu katika toleo hili la pili la Riziki 2024 ni agizo la Yesu, “Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu”. Lengo kuu la mada hii ni kukumbushana wajibu aliotuachia Bwana wetu Yesu Kristo wa kuihubiri

Injili kwa watu wote. Anawatuma watu wote walioko tayari katika kufanya utume huu mkuu.

“Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.” Huu ni mshangao wa walioitikia wito wa Bwana Yesu wa kuwafikia watu wote kwa Injili. Utapata kusoma pia habari za mmoja aliyeitika alipotumwa kwenda kuhubiri Injili katika nchi ya mbali, na jinsi ambavyo Mungu alikuwa pamoja naye. Je, uko tayari kusema, “Niko hapa Bwana, nitume mimi”?

Yaliyomo:

Uk. 3-5: Enendeni mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi

Uk. 6-7: Wanafunzi sabini waliotumwa

Uk. 8-10: Nitume mimi

Uk. 11-13: Uzoefu wangu kama mmisionari

Uk. 14-15: Tunawafikiaje wasioamini?

Enendeni mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi

Kati ya mambo magumu, lakini yenye manufaa na ufanisi mkuu katika maisha ya jumuiya ya wanaomwamini na kumfuata Yesu Kristo, upo wito wa kuwa wanafunzi wanaowafanya wengine nao wawe vivyo hivyo.

Kuwa mwanafunzi wa Yesu

Ili kupata uelewa wa ndani wa agizo la Yesu katika Mt 28:1-20, ni muhimu kuelewa maana ya maneno haya “mwanafunzi” na “uanafunzi”.

Maana ya kawaida, jinsi maneno yanayofahamika, kutumika na kuzoeleka na jamii, ni kwamba mwanafunzi ni mtu yeyote anayejifunza elimu au kazi fulani. Na uanafunzi ni hali ile ya kuwamo katika mafunzo.

Maana hizi hazihusiani moja kwa moja na maana ya ujumbe unaojadiliwa katika makala hii. Kuna neno la tatu linalohitajika pia, ambalo linatakiwa kufafanua zaidi maana hizo, kama tukitaka kuelewa maana ya kuwa mwanafunzi wa Yesu. Ni neno “ufuasi”.

Kwa kufuata Maandiko Matakatifu, kuwa mwanafunzi wa Yesu ni zaidi ya ile hali ya kujifunza. Kibiblia kuwa mwanafunzi hakuachani na ufuasi. Mwanafunzi ni mtu anayemfuata Yesu Kristo kwa imani kama Mwokozi wake, tena Bwana wake. Maisha yake yanafungamana na maisha ya Yesu na kuongozwa katika yote na mafundisho yake.

Watu wengi wamezoea kwamba “wanafunzi” ni wale kumi na wawili ambao pia wameitwa mitume. Hii ni kwa kufuata

Biblia. Lakini maana yake haiishii hapo. Inawahusu Wakristo wote. Mtu asipokuwa mwanafunzi wa Yesu kwa maana hiyo ya kibiblia, siye Mkristo wa kweli. Kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo kunahusu si tu kufunzwa naye mambo fulani, bali pia kufikia hatua ya kuyaamini, kuyategemea na kuyaishi. Kunahusu hata kuyatekeleza kwa kuitikia wito wa Yesu wa kuwafanya wengine kuwa wanafunzi na wafuasi wake. Huo wito ni mwito na wajibu wa ki-Mungu unaomaanisha kushiriki utume na misioni ya Mungu.

Mamlaka ya anayeagiza

Anayeagiza utendaji huu ni mwenye mamlaka. Ndiyo mamlaka aliyopewa na Mungu baada ya kufufuka. Si mamlaka ya kidunia bali ni uweza wa ki-Mungu unaoenea hapo ng’ambo ya kaburi. Imekwisha kazi ya Yesu kuwa Mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu na kuiondoa kati ya Mungu na sisi binadamu (Yn 1:29). Amebatili mauti na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili (2 Tim 1:10).

Sasa Yesu anaagiza kwamba habari hii njema ifikishwe hadi ya miisho ya dunia. Anaowatuma ni wanafunzi wake. Haiwezekani kuwaleta wengine kwa Yesu Kristo pasipo kwanza kuketi chini ya miguu yake ili ufundwe hadi ujumbe huo uwe ushuhuda wa maisha yako. Ukishafundika hivyo, ndipo unatumwa kuwafunza wengine. Hii si kanuni ya ualimu wa kawaida, bali ni wito wa aliyetufanya kuwa wanafunzi wake na kutupatia

3 2 RIZIKI TOLEO 2, 2024 RIZIKI TOLEO 2, 2024
MADA TAHARIRI

neema na baraka ya kuwaita wengine kuja kuwa wanafunzi wake vilevile.

Mwito huu unafuata baada ya sisi kuokolewa, na unatuingiza katika huduma takatifu ya ki-Injili. Yesu anatuita kwenda kuwaleta mataifa, yaani wale wasiomjua, wamwamini kuwa ndiye mwokozi wao.

Huwezi kufanikisha huduma hiyo pasipo kwanza kujikabidhi katika mapenzi ya Mwokozi wako na kuyaweka maisha yako katika uongozi wa Bwana wako (Rum 12:12). Huwezi kuwafanya wengine kuwa wanafunzi pasipo wewe mwenyewe kuishi hivyo na Kristo. Kwa upande mwingine, kukubali mamlaka na uongozi wake katika kila hali ya maisha yetu kunatufanya tuwe tayari kuwafunza wengine. Hata maisha yetu hushuhudia mamlaka ya Yesu ya kuwaokoa na kuwapa uzima watu wote.

Mwalimu wa kweli

hivyo. Kristo yupo hivyo, basi hatuwezi ila kuishi kama yeye. Tafakari Yn 13:1-15.

Uanafunzi wa Yesu

Kuna tofauti kubwa mno kati ya uanafunzi wa kiulimwengu na ule wa Yesu Kristo. Mwalimu wa elimu ya kidunia halazimiki kuyaishi anayoyafundisha. Siyo lazima tabia yake iakisi mafundisho anayotoa, wala hahusiki na maisha ya anaowafundisha. Wajibu wake ni kufundisha jambo fulani, basi. Sivyo mwalimu Yesu Kristo alivyo.

“hutaka watu wote waokolewe” (1 Tim 2:4)

Pengine utamaduni wa kiafrika unaweza kutusaidia kuelewa. Mzee anapokaribia kuondoka kwa njia ya kifo, huwapa maneno ya baraka na mwongozo wa maisha kwa wanaobaki nyuma yake. Hapa Yesu Kristo ni zaidi ya Mwafrika anayeaga dunia. Anatupa maneno ya baraka na mwongozo wa maisha yetu kama huyu aliyekufa, lakini tazama, yu hai na kuongozana nasi daima.

Kuna tofauti kuu na dhahiri baina ya uongozi na ualimu wa watawala na walimu wa kidunia na uongozi na ualimu wa Yesu Kristo. Hao wa kidunia hutumia ukali na wana kujikweza na kiburi. Hivyo wanakosa sifa ya ualimu wa uhakika na ukweli unagusa moyo.

Kinyume chake, Yesu Kristo hutumia upendo na ni mwenye tabia ya upole na unyenyekevu. Mwelekeo huu unatufanya kuwa tayari kufunzwa naye na kumkabidhi maisha yetu ayatumie apendavyo.

Kwa nini? Kwa sababu anavyotutendea kwa upendo inatugusa hadi mioyo yetu na kutuvuta kufuata kielelezo chake. Tena upendo wake unatuwezesha kufanya

Waafrika wa asili huyazingatia mno maneno ya mtu aliyekufa. Hata huyatekeleza kwa umakini mkubwa. Ambao hawakuwepo alipokufa huwauliza waliosikia alisema nini kabla ya kufariki. Hufanya hivyo ingawa hakuna mzee wa kiafrika ambaye kufa kwake kunaweza kulinganishwa na kifo cha Yesu Kristo. Ubainifu wa tofauti hiyo utusaidie kupokea vizuri agizo la Yesu. Ametuachia ujumbe mzito sisi tulio wanafunzi na wafuasi wake. Tuna wajibu wa kuwafanya watu wote kuwa wanafunzi wake. Tena ametuachia maelezo tunayohitaji ili

kutekeleza wajibu wetu kiutendaji.

Tuutendee kazi kwa mfumo gani?

Kwanza tuwaendee hao ambao bado sio wanafunzi wa Yesu ili kumshuhudia. Kisha tuwabatize wale wanaovutwa na Injili, na kuendelea kuwafundisha hao waliobatizwa yale yote tuliyopokea sisi wenyewe kutoka kwa Yesu. Kwa maneno na maisha yetu tuwafundishe kuyaamini, kuyategemea, kuyatii na kuyaishi yote aliyoagiza Yesu Kristo.

Mataifa yote

Tukisoma Mt 10:5-6, tunaona jinsi Yesu alivyowatuma wanafunzi wake wa kwanza, akiwaagiza wasiende katika njia ya mataifa wala wasiingie katika mji wowote wa Wasamaria. Waende kwanza kwa Wayahudi tu.

Ipo tofauti kubwa Yesu anapowaagiza baada ya kufufuka kwake. Yametokea mageuzi makuu. Sasa Yesu ni Bwana wa dunia aliyekufa kwa ajili ya dhambi ya watu wa mataifa yote. Yote yako tayari kwa ajili ya kuwaingiza katika ufalme wake.

Si jambo jipya kabisa, kwa sababu kwenda kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wa Yesu ni wito unaoturejesha katika Agano la Kale (Mwa 12:3; Isa 25:6; 56:3-7; Mal 1:11). Hata hivyo ni kama uamsho mpya, Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo anapothibitisha mpango huo wa wokovu wa Mungu na kuuendeleza katika Agano Jipya (Mdo 10:34, 35; Rum 3:29-30; Gal 3:28). Kristo analeta ulimwengu wote pamoja akisema wote wawe wanafunzi wake.

Injili ilikuwa na mahali pa kuanzia. Kufuatana na mapenzi ya Mungu ilipaswa ianze kwa Israeli ya kale. Vilevile ni mapenzi ya Mungu sasa, kwamba ufufuo wa Kristo unaitoa Injili katika mipaka ya Kiyahudi (yaani ya kitaifa) na kuipeleka katika mataifa yote duniani. Mungu,

Muumba na Mwokozi wetu, “hutaka watu wote waokolewe” (1 Tim 2:4).

Itikio la uanafunzi wetu Ujumbe wa Injili hauwezi kufika kote alikokusudia Kristo isipokuwa kila Mkristo atakubali kuwa mwanafunzi wa Injili. Itikio au tokeo la uanafunzi litawaleta mataifa yote kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo mfufuka! Haiwezekani wewe kuwaleta wengine kwa Kristo kama hujawa kwanza mwanafunzi mwaminifu na mtiifu wa mtumaji.

Injili inayoweza kumfanya mtu awe mwanafunzi, ni ile inayomtambulisha Kristo kwa ulimwengu kuwa yeye pekee ndiye ambaye Mungu amemtuma kusema nasi. “Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa namna nyingi , mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika mwana aliyemweka kuwa mrithi wa yote tena kwa yeye aliufanya ulimwengu” (Ebr 1:1-2).

Utekelezaji wa agizo kuu unaanzia kwenye itikio la kuondoka tulipo. Yesu anatutuma. Hawaji wenyewe, lazima tuende kuwafanya walimwengu kuwa wanafunzi wake Kristo Yesu.

Huo ndio umishionari wa Injili. Ni muhimu na wa lazima kuliko kazi zote katika ulimwengu, kwa sababu wokovu wa watu waitegemea. Kimsingi ni kazi ya kushuhudia, na inategemea tu utayari wetu wa kumtii Bwana wa Kanisa kutumwa naye anakotaka yeye. Maana tukumbuke, hatupo peke yetu, bali ameahidi kwenda pamoja nasi, na kwamba kuna nguvu na uweza wa Roho Mtakatifu juu yetu tunapotafuta kutekeleza agizo lake.

5 4
RIZIKI TOLEO 2, 2024 RIZIKI TOLEO 2, 2024 MADA MADA
Mch. Oswald Ndelwa

Wanafunzi sabini aliowatuma Yesu

Kama leo Yesu angefuata kanuni za siku hizi za masuala ya ajira, orodha yake ya majina ya wanafunzi ingekuwaje? Bila shaka ingekuwa ya tofauti sana na ile tunayoisoma katika Biblia.

Vipi na Mitume wa Yesu?

Kwanza Yesu angewapa kipaumbele wana wa makuhani na si wavuvi, watu ambao huhesabika wenye maisha duni.

Kwa hiyo Petro, Andrea, Yohana na Yakobo wasingekuwepo kwenye orodha ya wanafunzi. Wala Yuda Iskariote! Mathayo, je? Huyu ni sawa. Lakini pengine alizoea kuiba ushuru? Basi, aondolewe pia kwenye orodha. Na vipi na wale wengine? Hakuna aliyekuwa na sifa za elimu. Wataalamu wangemshauri Yesu awatafute wengine, au atumie malaika.

Lakini kabla hatujakubali shauri hili, tutafakari zaidi. Leo hii Kanisa lake Kristo ulimwenguni kote linajivunia misingi iliyowekwa na hao walioonekana kama watu wa chini na wasiofaa.

Yesu Kristo hakurudi mbinguni kutafuta malaika wa kufanya kazi nao. Aliridhika kuwashirikisha watu wa kawaida kazi kuu ya kuieneza Injili, watu kama wavuvi, watoza ushuru, wasio na elimu, watu waliokulia vijijini n.k. Hao ndio waliofanya kazi hii kubwa ya kueneza Injili ambayo tunaishuhudia leo!

Walikuwa tayari kumfuata

Baadaye Yesu aliwatuma wanafunzi wengine sabini wamtangulie kwenye miji na vijiji, wakiponya watu na kuhubiri habari za njema za Ufalme wa Mungu (Lk 10:112). Je, hawa walikuwa na sifa gani?

Biblia haitaji majina yao wala vigezo vilivyotumiwa kuwachagua. Kwa nini?

Kwa sababu hazikuwepo sababu hizo maalumu tunazoziangalia sisi. Siyo mambo kama majina yao, familia walizotoka, taaluma zao, wala maisha yao ya awali, yaliyokuwa muhimu kwa Yesu. Hakuhitaji hata kuwahoji kabla wa kuwaita. Alijua wote walifaa. Wote walitosha. Ili kuwa wanafunzi na watumishi wake, Yesu alidai jambo moja tu kwao. Yesu alikuwa amewaita, “Nifuate”, wakamfuata (Mt 4:19-22; 9:9).

Kwa kumfuata Yesu, wale sabini walikuwa na nafasi ya kipekee ya kusikia mafundisho aliyoyatoa na kuona miujiza aliyoifanya. Kwa kusikia, kuona na kupapasa, walidhibitishiwa uungu wake, kwamba Yesu ni Kristo na Muumba wa vyote na Mwenye nguvu na mamlaka juu ya enzi zote na vyote vilivyoumbwa.

Walihitimu na kuwezeshwa kufanya mambo makuu kama mahubiri, ishara na maajabu kwa sababu moja tu ya kipekee, “Walikuwa pamoja na Yesu” (Mdo 4:13).

Walikuwa mashahidi

Hata baadaye wakati wa Mitume, ufuasi wa Yesu ulichukuliwa kuwa sifa za kipekee za kukubalika kuwa mtume au kiongozi katika kanisa la kwanza (Mdo 1:21-23).

Sharti moja lilikuwa la msingi. Kazi ya Injili ya wakati huo ilihitaji, si watu waliofundishwa na kumwamini Yesu tu, bali watu walioshuhudia kufa na kufufuka kwake.

Ni matukio hayo katika maisha ya Yesu yaliyowapa ujasiri na kuwafanya kuwa tayari hata kufa kwa ajili ya kazi ya

Injili. Na zaidi sana uliwapa kumtegemea

Yesu kwa mahitaji yao ya kila siku. Ndiyo sababu wale sabini walitii walipoambiwa wasibebe mfuko wala mkoba wala viatu vya akiba (Lk 10:4).

Walikuwa wameshuhudia uwezo wa Yesu, kwa mfano alipogeuza maji kuwa divai na kulisha maelfu jangwani kwa samaki wawili na mikate mitano, mlo uliomtosha kijana mmoja tu (Yn 2:1-12; Mt 14:16-21).

Walikwenda kwa kumtumaini Yeye anayevika maua ya kondeni uzuri unaopita fahari ya Mfalme Sulemani (Mt 6:25-26). Hawakuwa na shida ya kuishi kwenye nyumba yoyote waliyokaribishwa, wala kula chakula chochote walichoandaliwa (Lk 10:5, 7). Hawakuogopa kukataliwa (Lk 10:10).

Haya yote walikuwa wamefundishwa na kuyazoea katika shule ya kukaa na Yesu. Walikuwa tayari kwa lolote.

Tumeitwa kuwa mashahidi Kukaa pamoja na Yesu, na kujifunza kwa kusikia, kuona na kufanya, kuliwafanya wahubiri wakuu wa kwanza wa Injili. Kama asemavyo mmoja wao, walihubiri lile walilosikia kwa masiko yao na kuona kwa macho yao, na lile walilotazama na kulipapasa kwa mikono yao (1 Yoh 1:13). Maana yake, kimsingi, mahubiri yao yalikuwa ni ushuhuda.

Hatujaitwa kufundisha theolojia na kuwafanya wengine maprofesa wa theolojia. Tumeitwa kushuhudia alivyotutendea Yesu. Kila mfuasi wa Yesu anaweza kushuhudia jinsi utu wake wa asili ulivyomfanya mtumwa wa dhambi, na jinsi alivyoshindwa kujinasua kutoka kwenye kongwa la dhambi na adhabu yake. Kila

mfuasi wa Yesu anaweza kueleza alivyopata kusikia na kuamini habari za Yesu anayewapenda wenye dhambi, na jinsi alivyowekwa huru kwa kupokea bure msamaha wa Yesu Kristo.

Tumezoea kusema, “Aliye na Mwana (Yesu), ana ushuhuda!” Msemo huu unatumika tunapowaita watu washuhudie matendo makuu ya Mungu kwenye maisha yao. Ni sawa kabisa kushuhudia kwa Wakristo wenzetu. Lakini kupitia habari za hao sabini tunaitwa kushuhudia hasa kwa wasiomwamini Yesu, watu waliofungwa na dhambi na kuendelea kuteswa na shetani, watu ambao hawana tumaini la uzima wa milele.

Ushuhuda wa maneno na matendo

Tumezoea sana ushuhuda wa maneno, lakini tusisahau kwamba matendo yetu na maisha yetu ya kila siku ni mahubiri yenye nguvu, hasa kwao wasioamini. Tena, siyo kila mfuasi wa Yesu aliye na kipawa cha kuhubiri. Sawa! Lakini wote wamwaminio Yesu anawapa kuwa chumvi na nuru kwa majirani zao (Mt 5:13-16). Maana yake, kila Mkristo anayo nafasi na wajibu wa kumtangaza Kristo kwa neno na kwa matendo yake.

Hivyo basi, kazi ya kueneza Injili siyo ya wachungaji na wainjilisti tu. Wewe na mimi tuna wajibu wa kuwafikia majirani wanaotuzunguka. Tena kumbuka, wito wa kueneza Injili ni kwa kila mfuasi wa Yesu, watu wa kawaida. Ufuasi wa Yesu ndio cheti cha pekee unachohitaji ili kuwa shahidi wake. Mahitaji mengine umwachie Yesu.

Mch. Gideon Mumo

7 6 RIZIKI TOLEO 2, 2024 RIZIKI TOLEO 2, 2024 WATU WA BIBLIA WATU WA BIBLIA

Nitume mimi

Mungu ni Muumbaji wa kila kitu. Kwa siku sita aliviumba vitu vyote. Lakini vyote havina thamani sawa. Ukisoma Mwanzo 1 utagundua kuwa uumbaji huu una kilele chake. Ni pale Mungu alipomwumba mtu, kiumbe chenye sura na mfano wake Mungu mwenyewe ili awe wakili juu ya kazi yake. Ndiyo maana Mungu hakuendelea na uumbaji mwingine tena baada ya ku-mwumba mtu siku ya sita. Badala yake, kwa kuibariki siku ya saba na kuitakasa, alimkaribisha mtu katika ushirika wake wa karibu.

Kitendo cha Adamu na Hawa kukiuka maagizo waliyopewa na Mungu (Mwa 3:1-6) kiliwafanya wapoteze nafasi hiyo, pamoja na mamlaka, heshima na utu wao. Tunaona matokeo mawili tofauti katika habari zinazofuata, yaani hasira ya Mungu na upendo wake. Hasira yake ni pale alipomlaani nyoka (Mwa 3:14) na kumfukuza huyo mtu (Mwa 3:24). Hata hivyo upendo wa Mungu kwa mtu ni mkubwa zaidi, maana Mungu aliondoka akamtafuta, akamwita akisema, “Adamu, uko wapi?”

Mwanzo wa umisheni

Je, umeona na kuelewa? Huo ndio mwanzo wa umisheni! Na huo umisheni wa Mungu unaendelea katika Biblia nzima. Kama Mungu alivyoahidi tayari siku ya anguko la kwanza (taz. Mwa 3:15), lengo lake, Yesu alipokuja ulimwenguni, lilikuwa hilo hilo la kutafuta na kuokoa kilichopotea (Lk 19:10). Mpango wake na utekelezaji wake umeelezwa kwa ufupi katika Yn 3:16.

Tangu siku ya kufufuka kwa Yesu hadi

leo Mungu ameendelea kutumia mashahidi wa wokovu wake kwenda kuwaambia watu habari yake njema: “Mmeokolewa kwa neema, rudini sasa nyumbani kwa Baba! Mwurudie ushirika huo wa karibu na wa upendo mlioupoteza Edeni.”

Wito wa waumini wote

Mwaliko huu mwema unakuja daima pamoja na wito kwao wanaorudi kwa

Mungu: “Mwe sehemu ya wavuvi wa wengine. Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wana wa Mungu na wanafunzi wa Yesu.”

Umeitwa na Mungu! Lakini je, umeshindwa kupambanua sauti ya mwitaji? Au pengine hata unatafuta kujiepusha? Jifunze kwa habari ya kuitwa kwa Samweli. Ingawa hakuelewa kwanza alikuwa tayari, na baadaye aliposaidiwa na Eli aliuelewa wito wa Mungu, akafuata maelekezo kwa uaminifu (1 Sam 3).

Wito na utumishi

Neno “wito” ni kitenzi cha “kuita”. Tunaweza kuitwa kwa njia mbalimbali, lakini wakati wowote wito unakuja na uwezekano wa kujibu kwa njia mbili tofauti. Unaweza kuitikia ama kukaidi. Unaweza kukubaliana na unachoambiwa kufanya au kukipuuza (tafakari alivyojibu Yona, hasa katika Yon 1 na 3).

Kwa hiyo kuitwa ni jambo moja, kukubali wito ni jambo la pili, na kutekeleza ulichoambiwa kufanya ni jambo la tatu linalotakiwa kufuata. Na jambo kuu katika yote ni kuendelea kudumisha uhusiano na Mungu anayekutuma tangu mwanzo hadi mwisho.

Mfano hai

Nitumie wito na utumishi wangu kama mfano wa maana na matokeo ya wito wa umisheni.

Mimi ni mchungaji katika Kanisa la Moravian Tanzania. Wito wangu wa kwanza ni pale nilipomkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yangu na kubatizwa katika mauti ya Yesu Kristo. Hapo maisha mapya yalianza ndani yangu (2 Kor 5:17).

Baadaye viongozi wa kanisa waliona nisichokijua ndani yangu, wakanituma kusoma uchungaji nikiwa kijana kabisa bila ndoa. Nilioa tu nikiwa mwaka wa pili wa masomo yangu.

Kwa bahati nzuri kanisa lilikuwa na utaratibu wa kuwasomesha wenzi wa wachungaji wanafunzi, angalau mwaka mmoja. Mke wangu alisoma kozi maalumu ambayo ilimsaidia sana kuielewa huduma ya kichungaji.

Mke wangu amekuwa baraka sana katika utumishi wangu. Bila kumung’unya maneno, hiyo ni hatua ya kwanza kabisa ya kanisa katika kuwaandaa watumishi wake. Nilifanya kazi kama mchungaji tukihamishwa toka usharika hadi usharika mwingine. Sikuwahi kufikiri kama ningetumwa nchi za nje kuhubiri Injili, nilijua wapo wenye vigezo. Kama baba mwenye familia nilipata changamoto kidogo, hasa za kimazingira wakati wa uhamisho (kwa mfano katika suala la joto na baridi). Lakini kwa upande wa mila na desturi haikuwa shida, maana wakati huo wote ilikuwa ni hapahapa nchini kwetu nilipofanya kazi.

Wito wa kwenda ugenini

Nilipopata barua ya kwenda Malawi kutumika kama mmisionari sikuamini ma-

cho yangu. Mke wangu aliisoma na watoto waliisoma, lakini sote tukategemea viongozi wamekosea jina.

Tulianza kujifungia ndani kwa hofu na woga. Ilikuwa kama ukipanga kwenda mahali kuchukua kitu na unasahau ulichoendea. Hali ya msongo wa mawazo iliendelea kuwa kubwa, hasa pale kimya cha viongozi wetu kilipoendelea. Lakini baada ya kimya cha muda mrefu viongozi wetu waliwasiliana nasi tena wakituambia kuwa tupeleke taarifa zetu ili mchakato wa kutafutiwa vibali uanze. Hapo tulianza kuamini kwamba kweli barua ya wito mpya imetulenga sisi.

Hofu yetu ilikuwa ikitokana na taarifa tulizoanza kuzisikia kuwa huko tuendako kuna njaa kali iliyotokana na ukame. Pia tuliogopa mazingira ya kazi yatakuwa magumu mno, vilevile mawasiliano kwa sababu ya lugha hasa kuwa nyingine, na watu toka Afrika Mashariki ni lazima wawe na chanjo ya ugonjwa wa homa ya manjano.

Viongozi wa kanisa walipoona tunaanza kuhuzunika badala ya kufurahia utume, walituita, wakatutia moyo na kutufanyia ushauri nasaha. Zoezi la kututafutia vibali likawa kama kufanya ‘outing’, kwa kuwa wakati fulani tulikaa hosteli kama familia mpaka vibali vilipotoka. Aidha tulitengenezewa mazingira mazuri ili kututia nguvu tusiogope vitisho.

Hofu ya familia

Kwa kweli tulihitaji kutiwa moyo, kwa sababu kila mmoja katika familia yetu alikuwa na hofu yake. Mke wangu alifikiria zaidi ugumu wa kuwaacha wazazi, ndugu na marafiki. Hili la kuwaacha watu wa karibu uliowazoea silo jambo jepesi. Linauma sana, hata ukijua na kukubali

9 8 RIZIKI TOLEO 2, 2024 RIZIKI TOLEO 2, 2024 IHUBIRI INJILI IHUBIRI INJILI

kuwa sasa basi utalazimika kuwatafuta rafiki wengine, maana utaishi mbali na wazazi.

Kuhusu mawasiliano mke wangu hakuifahamu lugha nyingine isipokuwa lugha za kitanzania. Swali lake lilikuwa: Nitaishije na majirani, hasa watu hawa wa kawaida? Maana alijua sio wote wanaojua lugha rasmi nchini Malawi ambayo ni Kiingereza.

Alijiuliza pia kuhusu hali ya uchumi. Kwenye vibali tulivyopewa imeandikwa kwamba haikuruhusiwa kufanya kazi nyingine mbali na ile iliyokuleta nchini, ambayo kwa upande wetu ilikuwa kuihubiri Injili. Wasiwasi huu ulikuwa mkubwa, maana yeye alikuwa mjasiriamali.

Watoto wetu waliogopa kupoteza marafiki. Itakuwaje na kubadilika kwa mtaala wa masomo? Wangejisikia upweke wakiacha majengo mazuri ya shule na walimu wao, makazi na hata mifugo?

Kwa ujumla hali yetu haikuwa nzuri. Kwa mtazamo wetu wa kibinadamu uhamisho huo ulikuwa mkubwa kuliko tulivyowahi kuhama maishani.

Tulivyoandaliwa na kanisa

Mbali ya maelezo niliyoyatoa hapo juu, kanisa lilituandaa kwa njia mbalimbali. Tulipata elimu ya theolojia na uzoefu wa kazi ya ufalme wa Mungu nchini Tanzania. Zaidi ya hayo kanisa lilituandaa kwa kututafutia vibali vyote vinavyohitajika kwa mmishenari, kama vile pasipoti, kibali cha muda cha kufanya kazi na chanjo muhimu.

Pia watoto wetu walipewa vibali, na walilipiwa ada katika shule ya binafsi. Kanisa mama walilipa pia mshahara na marupurupu kwa ajili ya kujikimu.

Tuliambiwa kutoa taarifa kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania ili tuweze kusaidiwa endapo kutatokea changamoto yoyote ya kiusalama. Na tuliaswa kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kulinda maadili ya kazi yetu.

Mambo ya kukumbuka kwa mmisionari

Kuna mambo mengi ambayo huwezi kuyaandaa kamili ukiwa bado nyumbani, na changamoto ambazo utazigundua tu baada ya kuhamia nchi nyingine. Hapa nitataja mambo manne ambayo tulijifunza ni ya msingi na kuzoea kwamba ukiyakumbuka vizuri yatakusaidia sana ukikaa ugenini:

Zingatia sheria za nchi. Usitegemee tu kwamba kama ukifanya jinsi ulivyozoea nyumbani, basi itatosha.

Uwe tayari kuendelea kujifunza. Pengine umejipatia elimu na uzoefu mkubwa na lengo lako ni kuwafundisha wengine. Lakini uendelee kuwa ‘mdadisi’ anayetaka kujifunza kazi, mila, desturi na utamaduni kutoka kwa wenyeji.

Zingatia wito wako. Ukifikia hatua ya kukata tamaa, kumbuka kuwa ndiye Mungu aliyekutuma kwa kusudi maalumu. Mwombe aendelee kukuongoza kulingana na wito aliokupa.

Endelea kuwaheshimu waliokutuma.

Hiyo utafanya kwa kuwapa taarifa mara kwa mara kuhusu maendeleo ya kazi na hali ya kifamilia. Hiyo utafanya vilevile ukitafuta ushauri wao badala ya kuamua wewe tu kwenye changamoto zinazokukabili.

Uzoefu wangu kama mmisionari

Tanzania huko Kyela. Lakini kwa muda wa miaka minane yeye na familia yake walikuwa wamisionari nchini Malawi. Tumemwomba ashirikishe baadhi ya mambo waliyozoea ambayo anaona ni muhimu wamisionari wapya na kanisa waliowatuma wazingatie.

Mpendwa, amini Mungu wetu yupo mahali popote uendapo, usihofu chochote. Sisi hatukupungukiwa kabisa ugumu, na vitisho aina nyingi hufungamana na maisha ya kawaida kabisa. Pia tukubali kuwa changamoto katika kazi ya Mungu zipo mahali popote.

Uzoefu wa familia yangu ni kwamba vitisho tulivyoambiwa vipo, hatukuwahi kuviona. Badala yake tulifurahia upendo na ukarimu wa wenyeji wetu.

Kila mahali kuna watu wakorofi, lakini Mungu aliendelea kutuepusha nao.

Mch. Rivas Kibona

Bila shaka ndiyo maana Yesu alisema, Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu (Yn 16:33). Tuliamini neno lake, badala ya kila wakati kuutazama na kuufikiria ugumu wa maisha.

Siyo hivyo tu, bali tulikuta pia kwamba mila, desturi na tamaduni zetu kama Waafrika hazitofautiani sana. Ukikazana kuwa mwenyeji katika nchi ya kigeni, inawezekana kabisa kupokea uzoefu kimazingira.

11 10 RIZIKI TOLEO 2, 2024 RIZIKI TOLEO 2, 2024 IHUBIRI INJILI KANISA LA NYUMBANI
Leo Rivas Kibona amerudi Tanzania akiendelea kutumika katika Kanisa la Moravian

Yawezekana kufanya kazi ya

Mungu popote

Unaweza kufanya kazi ya Mungu popote, kama haiingilii mifumo ya siasa ya nchi husika.

Zingatia kuwa elimu haina mwisho. Kadiri unavyokazana kujifunza ndivyo unavyopata uzoefu zaidi na kufurahia kukaa katika mazingira mapya. Uwe tayari kushirikiana na wenyeji wako.

Kama watumishi wengine wote wa kanisa, wamisionari wajitahidi kutunza kiapo cha uaminifu kwa Mungu na kutunza uhusiano mzuri na viongozi waliowatuma. Ushirikiano nao hutegemea kwamba wamisionari wanatoa taarifa ya kazi mara kwa mara.

Ili kazi ya umisheni ifanikiwe ni muhimu vilevile kwamba viongozi wa kanisa wana utaratibu wa kuwaita au kuwatembelea wamisionari ili kuwaondolea

upweke. Aidha wamisionari wawezeshwe kuwa na vikao, semina, warsha na mikutano yao ugenini. Pamoja na hilo ni muhimu kuangalia uwezekano wa wamisionari kushiriki mikutano ya watumishi wa kanisa na wenzi wao inayofanyika nchini mwao.

Kama mmisionari ana familia, basi mwenzi wake atunzwe kwa posho kama mtumishi mwenzi. Kwa kufanya hivyo itapunguza ukali wa maisha ughaibuni. Haki za mmisionari zisifutwe hata kama atapewa chochote ugenini.

Wamisionari ni wawakilishi wa kanisa lao na vilevile nchi yao ndani ya nchi ya kigeni. Kila wanalofanya lililo baya linaweza kuathiri ushirikiano, haijalishi huo ni wa kanisa mama na kanisa jipya au ni wa nchi yao na nchi waishimo. Kwa mfano tulijifunza kwamba muda wote tulipokuwepo nje ya vituo vya kazi ilikuwa

muhimu tusisahau kubeba vibali, maana vilihakikisha usalama wetu.

Wajibu wa kanisa katika kuwaandaa wamisionari

Ifahamike kuwa kufanya uinjilisti ni wajibu wa kanisa lote. Iwe mipango endelevu ya kufanya umisioni wa ndani na nje, maana kazi hii ndiyo uti wa mgongo wa kanisa.

Hiyo ni pamoja na kanisa kuwa na mahali maalumu pa kuandaa wamisionari. Kama hilo haiwezekani, basi kwenye vyuo vya kanisa kuwe na mtaala unaohusisha jambo hilo, hata kama ni kwa mwaka mmoja au mihula kadhaa tu.

Inapotokea watu fulani walio na sifa za kutumwa ugenini, ni muhimu kuhusisha familia nzima wakati wanapofanyiwa maandalizi ya kwenda kutumika hapo. Bila shaka matunda yake yataonekana, kazi hiyo inapofanyika kwa nguvu.

Watoto wasisahauliwe, maana ni sehemu muhimu ya utume huu. Waandaliwe

kiroho, kijamii na kisaikolojia kuhusu kuhama. Uzoefu wangu ni kwamba ule uhamisho wa ndani ya nchi waliopata kutokana na kazi yangu kama mchungaji, uliwasaidia baadaye tulipokaa ugenini. Mipango mathubuti ya uinjilishaji inafungamana na vitendo. Vipo vingi muhimu, kwa mfano kuandaa vibali kwa mtumishi na familia yake wanapotumwa ugenini. Izingatiwe pia jinsi wanavyoweza kupata likizo kama familia.

Jibu zuri kuliko yote

Kwa ujumla kazi ya umisionari ni nzuri, kwani ndiyo kazi tuliyopewa na Bwana wetu Yesu Kristo hapo anaposema, Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi (Mt 28:19-20). Tusizihofie nafsi zetu. Ndiye Mungu aliyetutuma, naye ameahidi kutulinda. Isitoshe, hata mazingira ya kazi na mawasiliano yamerahisishwa na utandawazi, tofauti na yalivyokuwa karne za 18 na 19.

Ni wajibu wa mtumishi kujilinda na dunia, maana akimwacha Kristo atatangaza Ukristo kama dini au ustaarabu mmojawapo tu. Wajibu wa mmisionari ni kuishi maisha yenye ushuhuda kwa watu, yaani uinjilisti wa matendo. Kumbuka sisi ni nuru ya ulimwengu (Mt 5:14).

Wainjilisti wameahidiwa donge nono: Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! (Rumi 10:15) Kwa hiyo nikuachie na swali hili la Mungu: Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? (Isa 6:8)

Uzoefu wangu ni kwamba hakuna jibu zuri kuliko hili: Mimi hapa, nitume mimi.

13 12 RIZIKI TOLEO 2, 2024 RIZIKI TOLEO 2, 2024 KANISA LA NYUMBANI KANISA LA NYUMBANI
Mch. Rivas Kibona

Tunawafikiaje wasioamini?

Wasioamini ni wale ambao sio Wakristo. Ni watu tunaoishi nao, majirani, marafiki, ndugu na jamaa. Ni watu tunaoshirikiana nao katika michakato ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii za maisha ya kila siku.

Kuwafikia kuna umuhimu gani?

“Tunawafikaje hao wasioamini?” ni swali la msingi na moja kati ya maswali muhumu mno kwetu sisi Wakristo wa leo, kwani uhai na ukuaji wa Ukristo hutegemea pia jinsi tunavyowafikiria na kuwafikia wasioamini. Hata kuna sababu nyingine yenye maana zaidi. Ninayofikiria ni wokovu wa hao watu. Hakuna mwokozi mwingine ila Kristo Yesu.

Wito wa kuwa mashahidi

Nikizungumza kimsisitizo, kazi ambayo Yesu aliwatuma wanafunzi wake kuifanya ni kuwa mashahidi wake kwa ulimwengu, wakianzia ‘Yerusalemu’ (yaani nyumbani) kwa hawa ambao hawakuwa wafuasi. Katika Injili ya Luka na kitabu cha Matendo, kushuhudia au kuwa mshuhudiaji ni hali isiyoweza kutenganishwa na wito wa kuwa mfuasi wa Yesu. Aliowaita ndio watakaomshuhudia. Luka ametumia neno “shahidi” kwa maana ya hali mbili. Kwanza kuhusu wale wanafunzi walioyashuhudia maisha ya Yesu tangu ubatizo wake hadi kufa na kufufuka kwake; pili kwa maana ya wale ambao walikiri, kuamini na kushuhudia baada ya kusikia ushahidi wa hao wanafunzi wa Yesu. Mitume wa Yesu walikuwa na wajibu maalumu, lakini aliposema, “Ninyi ni mashahidi wa mambo haya”,

hao Mitume hawakuwa peke yao. Tunafahamu wanafunzi wengine walikuwepo (Lk 24:33). Kwa hiyo utume wa Bwana Yesu ulikuwa kwa wote waliokuwepo pale. Na baadaye, siku ya Pentekoste, walikuwako wanafunzi 120 mahali pamoja; pia hawa wakawa mashahidi.

Kijiti kinakabidhiwa wengine

Stefano aliitwa kuwa shahidi wa Yesu (Mdo 22:20) ingawa hakuwa pamoja na Mitume walioshuhudia yote aliyosema na kuyafanya Yesu. Na baada ya muda mfupi tu Stefano akafa kifo cha hadhi ya kuwa shahidi. Maneno haya mawili “shahidi” na “mfia dini” yanatoka kwenye asili moja. Katika kipindi hicho kuwa shahidi wa Yesu ilimaanisha “kuwa tayari kuhatarisha maisha” au kuwa “shahidi wa damu”. Stefano hakusifiwa kuwa shahidi wa Yesu baada ya kuwa mfia dini kwa kuuawa kwa hadhi ya kishahidi, bali aliuawa kwa hadhi ya kuwa shahidi kwa sababu tayari alikuwa na kuishi kama shahidi wa Yesu.

Sisi tunapokeaji kijiti?

Ikiwa katika mazingira ya namna hiyo, Wakristo wa kwanza hawakuyahurumia maisha yao kwa habari ya kuwa mashahidi wa Yesu kwa wasioamini, sisi Wakristo wa leo tusemeje? Tutajiteteaje mbele za Yesu kwa kutowafikia hata majirani yetu na watu wengine tunaoishi nao karibu na katika mazingira mazuri ya amani? Hii ya kuacha tu kuwashuhudia ni hatari na ole kwetu, kama vile Mtume Paulo alivyosema, “Ole wangu nisipoihubiri Injili” (1 Kor 9:16).

Hatua za kuwafikia

Kwenye msingi huo wa kutambua umuhimu na ulazima wa kuwafikia wasioamini, hebu tuangalie sasa ni namna gani tutekeleze wito wetu tuliopewa na Yesu. Nitataja mambo matano:

1) Ni lazima kila Mkristo ajitambue kama mfuasi na shahidi wa Yesu. Kujitambulisha kuwa Mkristo ila hatuna ufahamu huo, ni kujidanganya. Hatua ya kuwa mfuasi wa Yesu ni muhimu. Tusikubali kubakia tu kujiita Mkristo kama tusipofanya chochote katika kuwafikia wasioamini. Neema kubwa tuliyopewa ya kuupokea wokovu bure katika Kristo inatutaka tuenzi badiliko hilo muhimu ambalo neema hiyo imefanya katika maisha yetu. Tumekuwa mashahidi wa Kristo kwa wasioamini ili nao wapate kuamini na kupokea neema ya Mungu inayotuokoa (Mdo 1:8).

2) Maisha yetu yaanze kuonesha kuwa sisi ni wafuasi wa Yesu kwa tabia na utakatifu, na tukubali gharama ya kujikana (Lk 9:23-25). Kwa maneno ya Yesu ni sawa na kukubali kuubeba msalaba na kumfuata yeye kila siku.

3) Kanisa liondoke kwenye mtazamo wa kutengeneza washirika tu. Badala yake, wawafanye watu kuwa wafuasi, maana wafuasi wa Yesu hawatakuwa watu tegemezi wanaokuja tu kuabudu, kutoa sadaka, kuimba na kuhubiriwa, bali pia watakuwa mashahidi wa Yesu kwa majirani zao ili idadi ya wafuasi wake iongezeke. Ni janga kubwa kuona kwamba Wakristo wengi hawajitambui hivyo.

Badala yake wanahangaika huku na kule kutafuta miujiza na injili ya mafanikio tu,

huku wakijikuta kwenye tanzi za matapeli na walaghai. Hii ni shida inayotokana na Kanisa kutowafundisha ufuasi, maana Wakristo hao wangejitambua kweli, hata wao wenyewe wangeweza kufanya ishara na miujiza. Kumbuka kwamba Yesu alisema, “Ishara hizi zitafuatana na hao waaminio”. Angalia neno hili la mwisho. Yesu hakusema ishara zitafuatana na mitume na manabii na wachungaji tu bali wote waaminio (Mk 16:17).

4) Kanisa liwatazamishe Wakristo kujihusisha na umisheni kwa kujitoa pamoja na vyote walivyo navyo ili kuwafikia wasioamini. Kanisa la sasa haliwafikirii wasioamini kwa uzito wanaostahili. Ndiyo sababu linabaki kuwa kama taasisi ya maendeleo tu, na si kama chombo cha Kristo kwa ajili ya kazi ya umisheni (Mt 28:19-20).

5) Kuwajengea uwezo Wakristo kwa njia ya mafundisho ya Neno la Mungu (Kol 3:16-17) ili waweze kuwajibu wale wa imani nyingine wenye maswali juu ya imani na tumaini letu (1 Pet 3:15-16).

Zingatia thamani ya uhai wako! Thamani na uhai wa Mkristo ni uwezo wa kushirikisha imani yake na kuwafanya wengine kuwa Wakristo, wafuasi wa Yesu. Vinginevyo ni Ukristo wa jina tu. Basi, kama wewe si mfuasi wa Yesu, ongea naye ili kuchukua hatua ya kumfuata leo.

15 14 RIZIKI TOLEO 2, 2024 JAMII RIZIKI TOLEO 2, 2024 JAMII
Mch. Goodluck Elias Msumari

Vitabu vya kukusaidia kuzungumza na rafiki yako mwislamu

Kamati ya Uhariri ya Riziki wanapenda kuwashukuru wasomaji wote waliochangia kwa utoaji wa gazeti. Asanteni ninyi nyote mliotuma hela, kuendelea kuombea maandalizi ya matoleo mapya, na kushirikiana nasi usambazaji wa Riziki. Mungu awabariki.

BIBLIA

RIZIKI TOLEO 2, 2024 SOMA
0759 544
Soma RIZIKI “online” www.issuu.com/riziki
917 S.L.P. 2696, Arusha editor.somabiblia@gmail.com www.somabiblia.or.tz
Soma Biblia inapendekeza

Turn static files into dynamic content formats.

Create a flipbook
Issuu converts static files into: digital portfolios, online yearbooks, online catalogs, digital photo albums and more. Sign up and create your flipbook.