RIZIKI TOLEO LA 4,2024

Page 1


RIZIKI

S.L.P. 2696, Arusha 0759 544 917

Barua pepe: editor.somabiblia@gmail.com

Kamati ya Riziki:

James Sabuni (mhariri)

Mch. Anza Amen Lema

Mch. Philip Bach-Svendsen

Cathbert Msemo

Mary Bura

Magreth Mushi

Mch. Gervas Meitamei Luhekelo Sanga

Waandishi walioshiriki:

Mch. Gideon Mumo

Mch. Morice Mapundi

Mch. Elitegemeo Y. Mpumpa

Kusirie Emmanuel Senkondo

Layout: Cathbert Msemo

Jalada: Cathbert Msemo

ISSN 2683 - 6491

Nakala: 5000

Usambazaji: SOMA BIBLIA

S.L.P. 2696, Arusha

S.L.P. 12772, Dar es Salaam

S.L.P. 1088, Iringa

S.L.P. 6097, Mwanza

S.L.P. 1062, Mbeya

S.L.P. 4231, Dodoma

www.somabiblia.or.tz

Neno la Injili kwa rika zote Tanzania!

Imechapwa na:

Imaging Smart Dar es Salaam

Unavukaje kwenye bonde?

Je, umewahi kupita katika nyakati ngumu kiasi cha kuona uko kwenye bonde la uvuli wa mauti? Wakati kama huo ulijisikiaje? Na ulikuwa unaona nini mbele yako? Katika maisha haya kupita au kupitishwa katika bonde la uvuli wa mauti si jambo la ajabu. Lakini swali ni je, unavukaje katika hilo bonde?

Rais Mstaafu Nelson Mandela amewahi kusema, “Hakuna njia rahisi mahali popote ya kupata uhuru, na wengi wetu inabidi tupite katika bonde la uvuli wa mauti tena na tena kabla ya kufika katika kilele cha kile tunachokiamini na kukitamani”.

Mada kuu katika toleo hili la nne la Riziki 2024 inasema, Katika bonde bado Mungu yupo? Ni swali ambalo ni muhimu kutafakari ili tuwatie moyo wale ambao wanapita katika hali ngumu na kukata tamaa. Ni msaada kwa wale ambao wanapita na watakaopita katika bonde la uvuli wa mauti na kuogopa kuwa hakuna tumaini tena kwa maisha ya mbele.

Ndani ya gazeti hili utakutana na kijana mmoja ambaye Mungu alimpaka mafuta kuwa mtawala angali mdogo.

Tokeo lake lilikuwa maisha yake kuwa hatarini, kwa sababu mtawala wa wakati ule alimwona kijana huyu kama adui.

Zipo pia makala mbalimbali na ushuhuda wa kukutia moyo kusonga mbele katika wito ulioitiwa, bila kujali hali unazopitia. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu” (Yn 16:33b).

Yaliyomo:

Uk. 3-5: Katika bonde bado Mungu yupo?

Uk. 6-7: Daudi: Bwana ni ngome na wokovu wangu

Uk. 8-9: Mungu Mtakatifu ana watoto wasio watakatifu?

Uk. 10-11: Krismasi - sikukuu ya nuru

Uk. 12-13: Usinipite Mwokozi

Uk. 14-15: Usimkatie tamaa mtoto

Katika bonde bado Mungu yupo?

Maisha yanaweza kuwa na changamoto nyingi zinazotufanya kuhisi kwamba tupo katika bonde la giza. Katika safari ya maisha tunakutana na nyakati za furaha, lakini pia majanga. Kinachowaletea wale wanaomwamini Kristo Yesu shida zaidi katika changamoto hizi ni kwamba hatumwoni Mungu tunapokuwa bondeni. Ni kana kwamba hayupo pamoja nasi, na bila Mungu hatuna tumaini.

Katika hali hii tusisahau kwamba tunazungukwa na kundi kubwa la mashahidi katika Biblia na historia ya kanisa.

Tunaweza kuona jinsi Mungu alivyojidhihirisha kwao katika nyakati ngumu, na jinsi imani yao ilivyowapa matumaini.

Katika makala hii tutaangalia mifano michache. Kwa sababu Mungu ni yeye yule jana na leo na hata milele, mifano hii inaweza kutupa mwangaza na matumaini katika safari yetu ya imani.

Fimbo na mkongojo

Daudi aliona magumu mengi katika maisha yake. Mara kwa mara alipita katikati ya bonde la uvuli wa mauti. Katika Zab 23 anatoa ushuhuda wake kutokana na maisha yake na Bwana kama mchungaji wake. Tafuta kwanza kusoma pole pole zaburi hii nzima, kisha endelea na makala hii.

Ni nini kinachomfanya Daudi kumwambia Mungu: Nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami (m.4)? Ni vifaa vile alivyovitumia Mungu,

ama gongo na fimbo au fimbo na mkongojo. Kama mchungaji mwema alitumia vifaa hivi kumlinda Daudi dhidi ya adui zake na kumrudisha kwa upole wakati wa Daudi kutetereka (m.5-6). Daudi akiendelea kukaa nyumbani mwa Bwana, nafsi yake ilihuishwa tena na tena na wema na upendo wa Mungu. Hii inatufundisha kwamba hata giza la maisha si dalili kwamba Mungu hayupo, bali kwa kutupitisha gizani Mungu anaweza kuimarisha uhusiano wetu naye.

Kutoka mateso hadi heshima Yusufu alikumbana na changamoto kubwa za kuuzwa kama mtumwa na kuwa katika jela. Hata hivyo tunasoma kwamba Bwana akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi (Mwa 39:2). Katika Zab 105:19 tunaona kwa ufupi ni kitu gani kilichomsaidia Yusufu kuwa na imani hai. Alipita katikati ya mambo hayo magumu hata wakati wa kuwadia neno lake, ahadi ya Bwana ilimjaribu. Neno hilo ni ndoto zile ambazo Mungu alimpa kuota. Lilikuwa na ahadi, na kwa kweli Yusufu alijaribiwa katika kulishika neno hilo. Lakini yale aliyotangulia [Yusufu] kusema yalipotimia, neno la Bwana [pia] lilimthibitisha Yusufu (Zab 105:19 NENO). Yusufu alipoendelea kuwa na imani kwa Mungu, alisitawi katika imani hiyo na kupata kuona mkono wa Mungu ukiwa pamoja naye. Mungu alimwinua kuwa Waziri Mkuu wa Misri, lakini jambo kubwa kwa Yusufu lilikuwa kuthibi-

tishwa kwamba Mungu kwa kusudi lake jema alimpeleka mbele ya familia yake ili aweze kuwa chombo cha Mungu katika kuwaokoa (Mwa 50:19-21).

Imara katika majaribu

Ayubu ni mfano mwingine wa imani thabiti katika nyakati za majaribu. Alikumbwa na misiba mikubwa iliyojumuisha watoto wake, mali zake zote kupotea na yeye mwenyewe kuugua (Ayu 1:13-19). Hata hivyo, Ayubu alijibu kwa kusema: Bwana ametoa, Bwana ametwaa; Jina la Bwana libarikiwe (Ayubu 1:21).

Kutokana na misiba hiyo, Ayubu alipita kwenye giza kubwa la imani hadi kutaka kukata tamaa na kumshtaki Mungu kwamba amenyimwa haki zake. Lakini hatimaye Mungu alipomjibu, Ayubu alitulia.

Mungu alimponya na kumbariki zaidi kuliko alivyokuwa awali (Ayu 42:10). Lakini jambo kubwa zaidi ni jinsi imani yake ilivyohuishwa na kuimarika, kama Ayubu anavyoshuhudia mwenyewe akimwambia Mungu: Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; bali sasa jicho langu linakuona (Ayu 40:5).

Hii inatuonesha kwamba Mungu anaweza kumtunza na kumbariki mtu tena, hata baada ya majaribu makali.

Ujasiri wa kumtegemea Mungu

Danieli ni mfano wa ujasiri na imani thabiti katika Mungu. Hata alipokabiliwa na hatari ya kufa kwa kuliwa na simba, alibaki na imani kwa Mungu, na alikataa kuabudu sanamu (Dan 6:10-12).

Danieli aliamini kwamba Mungu aweza kuwasaidia watu wake katika hali zote

na kuwakinga na hatari na majanga, na kweli alipona kwa ulinzi wa Mungu (Dan 6:22).

Imara katika mateso kwa ajili ya Kristo

Mtume Paulo alikumbana na magumu mengi kwa ajili ya Injili, ikiwa ni pamoja na kupigwa, kuteswa na kufungwa gerezani. Hata hivyo aliendelea kuwa na matumaini na kumtegemea Mungu. Katika 2 Kor 4:8-9 ameeleza hali yake: Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi.

Ni nini kilichoendelea kumtia moyo na nguvu mpya? Soma na kutafakari kwa makini 2 Kor 4:16-18!

Imani katika nyakati za giza

Martin Luther alikumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa Kanisa Katoliki wakati wa Matengenezo ya Kanisa. Alikabiliana na hatari ya kuuawa, lakini alisimama imara kwa imani yake. Kama alivyosema: “Mimi ninasimama hapa; siwezi kufanya vinginevyo, Mungu anisaidie. Amina.”

Ujasiri wake na imani yake vilitokana na Luther kuongozwa na Neno la Mungu.

Mfano hasa ni Injili ya Rum 1:17: Haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake [Injili], toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani. Kwa kulishika neno hilo, Luther alileta mabadiliko makubwa katika historia ya Ukristo.

Mateso na ushindi

Yesu Kristo ni mfano muhimu zaidi wa imani thabiti. Alikumbwa na mateso makali, akihuzunishwa, kuchapwa na kufa msalabani (Mt 27:26-50). Lakini ni zaidi ya mfano bora. Mwenyewe ni chemchemi ya imani yetu na sababu ya matumaini yetu.

Kupitia mateso hayo, Yesu alitimiza mpango wa Mungu wa kuleta wokovu kwa wanadamu. Tunapozingatia maisha ya Yesu, na jinsi alivyoshuka hata kuzimu, tunahakikishiwa kwamba hakuna chochote kinachoweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu (Rum 8:39).

Sababu ni ushindi wa Yesu. Alifufuka, na sasa yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea (Rum 8:34).

Ushindi wake ndio ushindi wetu sisi tunaomwamini.

Basi, hata kama sisi tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa, tunashinda katika mambo hayo yote, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda (Rum 8:36-37).

Maisha yetu tukimtazama Yesu Katika maisha yetu ya kila siku, Mungu anaweza kujidhihirisha kupitia matukio ya kawaida kama vile kupata kazi baada ya kuhangaika kwa muda mrefu, afya bora baada ya kuugua, au msaada kutoka kwa watu wakati tunapohitaji sana. Hutokea pia kwamba tunakumbana na changamoto zinazozidi uwezo wetu na kutaka kutushinda kabisa. Lakini tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu, na kuzingatia alivyoustahimili msalaba na kuidharau aibu kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake kwamba atatuleta kwa Mungu, basi tunajua kwamba hata tunapopita katika mabonde yenye uvuli wa mauti hatujaachwa peke yetu, wala hatutabaki hapo, bali tutamwona kama alivyo na kupata kuwepo alipo yeye kwenye kiti cha enzi cha Mungu.

Ndiyo, ni kweli Mungu anaposema: Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu (Isa 41:10).

Mch. Elitegemeo Mpumpa

Daudi: Bwana ni ngome na wokovu wangu

Daudi alitiwa mafuta kuwa mfalme wakati Sauli akiwa bado kwenye utawala (1 Sam 16:13). Tukio hili pamoja na ushindi mkuu ambao Mungu alimpa Daudi dhidi ya Wafilisti - hasa aliposifiwa kwa kumwua Goliathi - lilimfanya Mfalme Sauli kumwonea Daudi wivu (1 Sam 18:8), kutokumwamini (18:9), na hata kumwogopa (18:12,15, 29), na kwa sababu hii alianza kutafuta ili kumwua.

Njama za Sauli

Mara mbili Sauli mwenyewe alijaribu kumwua Daudi kwa mkuki alipokuwa akimchezea kinubi, lakini Mungu akamwokoa (18:10b-11; 19:10). Mpango mwingine ulikuwa kumfanya Daudi kuwa kiongozi wa vita dhidi ya Wafilisti, Sauli akiwa na matumaini kwamba Daudi angekufa vitani (18:13, 17). Lakini hata huko, Mungu alimpa ulinzi na ushindi mkuu dhidi ya Wafilisti (18:27; 19:8; 23:5).

Njama hizi mbili ziliposhindwa, Sauli aliahidi kumwoza binti yake Mikali, kama Daudi atamletea mahari ya govi mia za Wafilisti (18:25). Huu ulikuwa ni mtego mkubwa kweli! Lakini Mungu alimpa Daudi ushindi, na akamletea Sauli si govi mia tu bali mara mbili ya alichotaka. Hivyo basi Daudi alipewa Mikali, binti Sauli, kuwa mkewe (18:27).

Mwisho Sauli aliamuru mwanawe Yonathani na watumishi wake wote kumtafuta na kumwua Daudi (19:1). Na je, utapataje kupona wakati baba mkwe na wote walio karibu nawe wamepewa amri na mfalme wakutafute na kukuua?

Kulindwa na Mungu na watu

Jambo moja linaloshuhudiwa kwa Daudi hata wakati huu wa dhiki kuu, ni kwamba BWANA alikuwa pamoja naye (16:18; 18:12). Mungu alimpa Daudi kuona kibali kwa watu wote katika Israeli na Yuda (18:5,16), nao walimlinda na kumtunza siku zote alipokuwa mafichoni.

Kwa mfano tunaona hivyo, Sauli alipotazamia mwanawe Yonathani amtafute na kumwua Daudi sawa na alivyoamuru. Tofauti na roho iliyokuwa na Sauli, Mungu alitia upendo wa ajabu kati ya Yonathani na Daudi, na kumfanya Yonathani mtetezi na mlinzi wa Daudi kwa kufichua siri na njama zote za baba yake dhidi ya Daudi (18:3; 19:2-5; 20:2, 9).

Si urafiki wa kawaida tu uliomfanya

Yonathani kumpa Daudi joho lake, mavazi, upanga, upinde na mshipi (18:4). Hata tendo hili linaashiria kwamba Yonathani alimkubali Daudi kuwa yule aliyechaguliwa na Mungu kuwa jemedari na mfalme juu ya Israeli.

Mfano wa pili ni Mikali, binti Sauli na mkewe Daudi. Siku moja Sauli alituma wajumbe kumvizia Daudi nyumbani kwake ili wamwue. Lakini kinyume na alivyotazamia baba yake, Mikali alimsaidia Daudi kutoroka kwa kumteremsha dirishani kabla ya wajumbe wa Sauli kufika (19:11-17).

Mfano wa tatu ni Samweli, mwamuzi na nabii wa Mungu. Daudi alipokimbia na kujificha alikumbuka ni nani aliyeianzisha safari yake, na alimwendea Samweli huko Rama (19:18). Lakini huko

pia Sauli alituma kikosi kumkamata

Daudi. La kushangaza ni kwamba badala ya kumkamata Daudi, wajumbe hawa waliingiwa na Roho wa Mungu na kujiunga na Samweli na wana wa manabii na kutabiri (19:20).

Kisha Sauli alituma kikosi cha pili, nao pia wakajiunga na wenzao kutabiri (19:21). Na je, walitabiri nini? Biblia haisemi walichotabiri. Lakini siyo ajabu ikiwa wote walitabiri juu ya Daudi kuwa mtiwa mafuta wa Mungu na mfalme mteule juu ya Israeli.

Sasa Sauli alipotambua wote wamekwama, aliamua kwenda yeye mwenyewe na watumishi wake. Lakini hata na yeye hakuweza kumkamata Daudi. Badala yake aliingiwa na Roho wa Mungu, akavua nguo zake, na kutabiri uchi mbele ya Samweli na Daudi mchana kutwa na usiku kucha (19:22-24).

Bwana ni nani kwako?

Je, kutokana na habari hizo tuseme nini kuhusu ulinzi wa Mungu kwetu?

Katika Zaburi 18 Daudi anaimba: “Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu (Zab 18:2). Na kwa kweli hakuna ila Yehova anayeweza kutuhakikishia ulinzi kama alivyompa Daudi. Kwao wanaomtegemea Yehova, atakuwa Mungu wao milimani, na Mungu wao mabondeni, tena Mungu wao mchana na Mungu wao usiku. Kwangu mimi binafsi, yeye ndiye Mungu na wokovu wangu. Kwa nini na wewe usimfanye awe Mungu wako leo? Kama uko tayari basi mkaribishe aingie ndani yako leo ili afanyike Bwana na mwokozi wako.

Mch. Gideon Mumo

Mungu Mtakatifu ana watoto wasio watakatifu?

Nilizaliwa na kukulia katika familia ya kawaida ya Kikristo. Nilibatizwa nikiwa mtoto na kuendelea kupata mafunzo ya Kikristo kupitia wazazi na ndugu wengine.

Baadhi ya mambo ninayoyakumbuka ya Ukristo wangu tangu utoto ni kujiunga na darasa la shule ya Jumapili. Nikiwa na miaka 10 nilishiriki kukariri mstari wa moyo kutoka Zaburi 103:13: “Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao”. Mstari huu ninaukumbuka hata leo.

Mwanzo mzuri

Baada ya hapo nilijiunga na vikundi vya kwaya na maigizo vya shule ya Jumapili. Kupitia vikundi hivi tulishiriki huduma mbalimbali kanisani kwenye ibada za watoto na hata ibada za watu wazima. Nilipenda huduma hizi, kwani kupitia hizo niliweza kusafiri na kwaya nje ya kanisa letu la nyumbani. Baada ya hapo nilipata mafundisho ya kipaimara na kubarikiwa. Vitu hivyo hapo juu vilinifanya kujisikia kuwa karibu sana na Mungu na kuwa Mkristo mzuri. Kuna mwaka tulitembelewa na mhubiri wa Injili kutoka Umoja wa Kujisomea Biblia. Alipohubiri kwenye ibada kanisani niliguswa na ujumbe wake, na alipotoa nafasi ya watu kumpa Yesu maisha, nami nilisimama na kuombewa. Lakini kwa sababu ya kukosa mafundisho na malezi ya kiroho sikuendelea vema na uamuzi huo. Wakati huo nilikuwa darasa la tano.

Maisha ya Kujichanganya Nilipofikia umri wa kuanza kupevuka, nili-

anza kujiingiza katika maisha mchanganyiko na vijana wenzangu tuliokuwa nao shuleni na kuishi nao jirani. Tulishiriki shughuli za kanisani, lakini pia tulikuwa na maisha ya dhambi, kwani tulikuwa na mahusiano yasiyo sahihi na mabinti. Tulijifunza pia kuvuta petroli na sigara, na tulikuwa wagomvi na kupigana kimakundi na vijana wengine mtaani, n.k.

Nilimaliza shule ya msingi, na Mungu alinipa neema ya kufaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Ufundi Tanga. Nilipofika huko, pamoja na kuendelea na masomo kama kawaida, nilijiunga na Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (UKWATA). Kupitia UKWATA nilishiriki kuimba kwaya, michezo ya kuigiza, “jiving”, na mengineyo.

Swali gumu

Nikiwa kidato cha pili nilichaguliwa kuwa Katibu wa UKWATA wa tawi langu, na wakati wa likizo nilihudhuria kambi ya vijana iliyoandaliwa na Umoja wa Kujisomea Biblia.

Moja ya masomo yaliyofundishwa ni somo la Utakatifu. Mwalimu aliyetu-

fundisha alitoa swali la kujadili kwenye vikundi. Swali hili liliuliza: “Je, inawezekana Mungu Mtakatifu akawa na watoto wasio watakatifu?”

Wakati wa majadiliano, mimi nilijijibu haraka kuwa inawezekana kabisa Mungu Mtakatifu kuwa na watoto wasio watakatifu. Hoja yangu kubwa ilikuwa kwamba, watu wote wameumbwa na Mungu kama alivyoniumba mimi. Na asilimia kubwa ya watu, nikiwemo na mimi, hatukuwa watakatifu. Kwa hiyo nikasema kuwa Mungu hawezi kukubali hasara ya kutukataa sisi aliotuumba, kwamba sio watoto wake eti kwa sababu tu sisi sio watakatifu.

Tulipoingia kwenye vikundi na kuanza kujadili, asilimia kubwa ya wachangiaji walisema kuwa haiwekezani Mungu

Mtakatifu kuwa na watoto wasio watakatifu. Walisema hili wakionyesha ushahidi wa kimaandiko. Hili lilinifanya kuogopa sana. Niligundua kuwa niko kwenye hatari kubwa sana ya kupotea na kuangamia.

Tuliporejea darasani kwenye mawasilisho, mwalimu naye alihitimisha vivyo hivyo kwamba haiwezekani Mungu Mtakatifu kuwa na watoto wasio watakatifu.

Hii ilinifanya kukosa raha sana na kuanza kutafakari maisha yangu kwa upya. Je, niendelee kuishi kama Mkristo wa kawaida tu bila Yesu ndani yangu, au niamue moja kwa moja kuendelea na maisha yangu ya dhambi? Baada ya tafakari ya kina niliona kuwa maamuzi haya yote mawili yatanipeleka kwenye hatari ya kwenda jehanam.

Uamuzi uliotoa amani Lakini kulikuwa na uamuzi wa tatu. Nao

ulikuwa kuamua kujitoa kwa Yesu bila kujichanganya na dunia. Huu niliuona kuwa uamuzi mzuri, kwani ungenihakikishia kuwa na usalama kwa Mungu.

Ila nilijiuliza: Je, nitaweza kuamua kuokoka kweli kweli na kuacha raha na tamaa za ujana? Niliendelea kutafakari hili hata nje ya vipindi vya mafundisho. Usiku, wakati wenzangu wameenda kulala, mimi nilishindwa kulala kabisa. Nilitoka nje ya mabweni nikaenda barazani nikamwomba Mungu anisamehe na kumwambia: “Mungu, kama kweli wewe unaokoa na hao wanaosema wameokoka wameokolewa na wewe, basi naomba na mimi uniokoe, na unisaidie kubadilika kabisa nisirudi tena katika maisha ya mchanganyiko kama huko nyuma”. Maneno haya yalikuwa sala ya maana kwangu, maana nilienda kulala, na nilipoamka nilisikia amani kubwa. Mungu amenipa uhakika kuwa amenisikia na kunisaidia haja yangu niliyomwomba. Hali ya kuhukumiwa moyoni mwangu iliisha, na nikawa na uhakika na ujasiri kuwa nimesamehewa dhambi na kuokolewa.

Baada ya hapo niliendelea kushiriki kufanya huduma kwa wanafunzi, na mwishoni mwa miaka ya 1990 kwa neema ya Mungu tulianzisha huduma ya WanaUKWATA Washirikishwa (Senior Friends) ambayo imekuwa ikiwalea wanafunzi walioko mashuleni. Lakini pia imetusaidia na sisi kuendelea kumwishia Kristo kwa kusaidiana mahitaji ya kiroho na kimwili wakati huohuo tukiwasaidia wanafunzi.

Kusirie Emmanuel Senkondo

Krismasi - sikukuu ya nuru

Krismasi ni moja ya sikukuu maarufu katika utamaduni wa Kikristo. Sikukuu hii pia hujulikana kama Noel. Wakristo husherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo ambaye ni Mwokozi wa ulimwengu, aliyezaliwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Sikukuu hii husherehekewa tarehe 25 Desemba kila mwaka kwa kanisa la Magharibi na tarehe 6 Januari kwa kanisa la Mashariki.

Asili ya jina “Krismasi”

Kwa Kiswahili kuna majina mawili yanayotumika kwa sikukuu hii. “Krismasi” ni jina linalotokana na neno la Kiingereza “Christ Mass” lenye maana ya ibada ya Kristo, ambayo wengine huita Misa.

Jina la pili, “Noeli”, hutokana na neno lingine la Kiingereza “Noel” au “Nowel” ambalo limekopwa kutoka katika lugha ya Kifaransa (“Noël”), ambalo tena ni ufupisho wa neno la Kilatini “Natalis (dies)” lenye maana ya siku ya kuzaliwa.

Kutokana na asili ya neno Krismasi, tunapata kufahamu kuwa Krismasi ni sikukuu maalumu ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Historia fupi ya sikukuu ya Krismasi

Krismasi ni sikukuu ya zamani sana katika Ukristo, ila haikuwepo tangu mwanzo, wala hakuna uhakika hasa ni lini ilianza kusherehekewa.

Tarehe halisi ya kuzaliwa kwa Yesu haijulikani, kwa sababu utamaduni wa Kiyahudi wakati ule haukuwa na sherehe au kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa.

Ukristo ulipoenea katika dola ya Rumi

kati ya mataifa yenye desturi ya kusherehekea siku ya kuzaliwa, pia siku ya kuzaliwa kwa Kristo ilianza kusherehekewa. Hapo ndipo asili ya sikukuu ya Krismasi.

Suala la tarehe

Tofauti ya tarehe hutokana na kugawanyika kwa kanisa katika sehemu mbili: Kanisa la Magharibi, ambalo hujumuisha

Kanisa Katoliki (la Kiroma) na makanisa ya Kiprotestanti, na Kanisa la Mashariki, ambalo hujumuisha makanisa ya Kiorthodoksi. Mwaka 1054 BK hutajwa kama mwaka rasmi wa tukio hilo, lakini vyanzo vya mgawanyiko huo vilionekana mapema zaidi. Makao makuu wakati ule ya sehemu hizo mbili za Ukristo yalikuwa mji wa Roma huko Italia na mji wa Constantinople ambao ni sawa na Istanbul huko Uturuki siku hizi.

Sasa historia hutuambia kuwa Kaisari

Eliogabalus, ambaye alizaliwa Syria na kutawala Rumi 218-222 BK, alianzisha sherehe ya sikukuu ya “kuzaliwa kwa Jua” huko Rumi. Mwaka 273 BK Kaisari Aurelius akaithibitisha rasmi kuwa sikukuu ya taifa. Sikukuu hii huitwa “Sol Invictus”, jina linalomaanisha “jua lisiloshindika”. Hii ilikuwa ibada iliyoingia Rumi kutokea Uajemi (Iran) ambako mungu Mithra aliabudiwa kama mungu wa nuru.

Kipindi cha utawala wa Kaisari Licinius (308-324 BK) sikukuu hiyo ilikuwa bado ikiadhimishwa tarehe 19 Desemba, lakini baadaye ikahamishiwa kufanyika tarehe 25 Desemba.

Wataalamu mbalimbali hudai kuwa kanisa liliweka sikukuu ya Kristo kwenye tarehe hiyo, yaani 25 Desemba, kwa nia

ya kufanya ichukue nafasi ya sikukuu ya jua kama mungu.

Sababu za kuabudu jua

Katika dini za asili za Kiafrika kuna vidokezo kwamba jua liliangaliwa kama mungu, tena mungu mkali.

Sababu ya sikukuu hiyo ya jua kama mungu ni tofauti. Waumini wa dini Jua waliona wakati wa Desemba kama kipindi cha pekee, maana katika nusu tufe ya kaskazini ya dunia urefu wa mchana unapungua kuanzia mwezi wa Juni hadi tarehe 21 au 22 ya Desemba ambapo nuru ‘inarudi’ tena na mchana huanza kuongezeka. Mwendo huo wa jua ulichukuliwa kama ushindi wa jua, yaani ushindi wa nuru dhidi ya giza.

Nuru kama ishara ya Kristo Biblia humfananisha Kristo na jua. Hii imetajwa katika sehemu mbalimbali za Maandiko Matakatifu.

Katika Agano la Kale kujiliwa na Bwana kunafafanuliwa kama kuangazwa na nuru (taz. Hes 24:17; Isa 60:1), na katika Isa 9:2-6 kujiliwa huko kumeunganishwa na habari ya kuzaliwa kwa mtoto. Tena katika Mal 4:2 tunakuta unabii au ahadi juu ya tukio hilo: Kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia; lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama mazizini.

Katika Lk 1:78 baba yake Yohana Mbatizaji anamsifu Mungu kwa sababu sasa ahadi hiyo imekaribia kutimia. Anamwambia mtoto wake kwamba atatangulia mbele za uso wa Bwana na kumtengenezea njia yake. Matokeo yake yanaelezwa hivi: Kwa [njia ya rehema za

Mungu] mwangaza utokao juu umetufikia. Maana yake ni wokovu unaopatikana kwa njia ya kusamehewa dhambi. Jua lililoumbwa na Mungu siku ya nne halitadumu milele, lakini Kristo kama nuru ya watu wake atakaa milele: Mji ule [wa Yerusalemu mpya] hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu hutia nuru, na taa yake ni Mwanakondoo.

Tukumbuke kuwa maneno hayo yote yameandikwa muda mrefu kabla ya kutokea kwa sikukuu ya Sol Invictus. Maana yake ni kwamba Wakristo tunamwabudu Kristo Yesu kama ‘Jua la kweli’, tukiamini kuwa ndiye Nuru ya kiroho ya ulimwengu na mwangaza wa rehema na utukufu wa Mungu.

Kristo - ushindi wetu

Yesu mwenyewe anauthitishia ulimwengu kuwa Yeye ndiye nuru yake, na mtu atakayemfuata hatakwenda katika giza la kiroho bali atakuwa na nuru na uzima (Yn 8:12). Huu ndio ujumbe wa Krismasi. Mungu ameweka mpango mahususi wa kututoa kutoka katika giza la kutomjua Mungu na kutuingiza katika pendo la Mwana wake, Yesu Kristo. Giza huashiria mauti wakati nuru huleta uzima kwa yule anayeamini.

Habari njema tunayoisherehekea sikukuu ya Krismasi ndiyo neema hiyo ya kutoka mautini kuingia uzimani ambayo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili (2 Tim 1:9-10).

Mch. Gervas Metamei

Usinipite Mwokozi

Katika maisha kila mmoja angependa kuwa na hali nzuri kila wakati. Ina-weza kuwa afya njema, uchumi mzuri, marafiki na familia bora, kazi nzuri yenye mshahara mkubwa na mazingira mazuri ya kazi na kadhalika. Lakini je, tukifanya wenyewe inatosha kuwa hivyo?

Ukweli ni kwamba tunapoishi hapa duniani changamoto mbalimbali zinatokea. Kuna wakati unajikuta katika shida inayokufanya kujisikia mpweke katikati ya wengine. Huu ndio wakati watu wengi hutamani kupata mtu mmoja wa kuwashika mkono na kuwasaidia kupita katika matatizo. Kwa sababu ya kujisahau na kufanya bidii kutafuta furaha katika mambo niliyotaja hapo juu tunajikuta tukiingia katika huzuni badala ya furaha.

Lakini ipo furaha ambayo inaweza kudumu maishani mwote. Furaha hii inatoka kwa Yesu pekee. Ili kuishi vizuri na kwa furaha, unahitaji kuwa naye, akuguse na kukusaidia katika kila hali.

Tunaweza kujifunza kupitia ilivyotokea mpaka kutungwa kwa wimbo maarufu sana ‘Usinipite Mwokozi’ au ‘Pass me not!’. Wimbo unapatikana katika vitabu vingi ikiwemo Tumwabudu Mungu Wetu namba 292 na Tenzi za Rohoni namba 10. Maneno ya wimbo huu yalitungwa na Fanny Jane Crosby. Alizaliwa mwaka 1820 nchini Marekani. Kabla hajafunga miezi miwili alipata shida kubwa ya macho. Bahati mbaya Fanny akatibiwa na mtu ambaye alijitambulisha kama daktari, lakini hakuwa na leseni ya udaktari. Alimpa matibabu yasiyo sahihi yakasababisha Fanny kuwa kipofu.

Akiwa na umri wa miezi sita tu, baba yake alifariki, akalelewa na mama yake pamoja na bibi yake. Alipofikisha miaka 15, Fanny aliweza kukariri katika Biblia. Wakati huo alijiunga na taasisi ya watu wenye ulemavu wa kuona, akasoma na kumaliza akiwa na miaka 27. Lakini aliendelea kukaa pale shuleni akawa mwalimu mzuri akifundisha Kiingereza, elimu ya Usemaji na Historia ya kale.

Alianza kutunga mashairi akiwa bado mtoto. Alitumia kipindi cha likizo kwa ajili ya kuandika mashairi ya kidunia ambayo yalipendwa sana kipindi hicho. Baada ya imani yake katika Yesu kuhuishwa upya, Fanny alianza kutunga nyimbo za kikristo.

Nyimbo nyingi alizitoa akitumia jina tofauti. Watafiti wanasema ametunga nyimbo kwa idadi kati ya 8000 na 9000. Baadhi ya nyimbo hizo zilitumika sana kwenye mikutano ya kiroho. Mmoja wapo ni huu Usinipite Mwokozi.

Utafiti unaonyesha kuwa, Fanny aliandika wimbo huu baada ya kutafakari kuhusu ziara yake gerezani. Kwa sababu ya umaarufu wake, mara nyingi alialikwa kwenye huduma za misheni. Katika hafla moja, alishiriki katika huduma ya misheni gerezani. Alimsikia mwanaume aliyefungwa gerezani akipaza sauti akisema, “Bwana, usinipite.” Alivutiwa sana na jambo hili. Ndipo akaandika maneno ya wimbo huu ‘Usinipite Mwokozi’. Wakati fulani Fanny alinukuliwa akisema, “Niliandika mistari huku kilio cha kusihi cha mwanaume yule kikiwa bado masikioni mwangu.”

Fanny Crosby aliweza kupiga kinanda, lakini hakutunga sauti za nyimbo zake. Mmoja aliyemsaidia sana na muziki ni ndugu William Kirkpatrick. Alikuwa fundi seremala, lakini baadaye akajikita katika muziki uliokuwa wito wake. Alitunga sauti za nyimbo zaidi ya 50, pamoja na kuwa mwalimu wa shule ya Jumapili na kwaya katika Kanisa moja kule Philadelphia.

Inawezekana yule mfungwa alijutia sana makosa yaliyompeleka gerezani au alihuzunishwa na kuwepo pale na inawezekana hata amesingiziwa. Lakini alitambua kuwa Yesu pekee anaweza kumsaidia. Na wewe una nafasi ya kutafakari unapoimba wimbo huu na kumwita Yesu awe nawe katika nyakati zote. Karibu tuimbe ‘Usinipite Mwokozi’.

Usinipite Mwokozi, Unisikie; Unapozuru wengine, usinipite.

Yesu,Yesu, Unisikie; Unapozuru wengine, Usinipite.

Kiti chako cha rehema, Nakitazama; Magoti napiga pale, Nisamehewe.

Sina ya kutegemea, Ila wewe tu; Uso wako uwe kwangu, Nakuabudu.

U mfariji peke yako, Sina mbinguni, Wala duniani pote, Bwana mwingine.

Cathbert Msemo

Usimkatie tamaa mtoto

Je, umeona wazazi wengine wakipata changamoto kwa sababu ya vijana wa kizazi hiki cha kidigitali kinachoitwa Gen Z (Generation Z au kizazi cha Z; ni sawa na waliozaliwa kuanzia mwaka wa 1990 mpaka 2010). Pengine wewe mwenyewe ni mmojawapo? Je, changamoto hizi zimekufanya kwa njia moja au nyingine kukata tamaa hata usiwe na matumaini tena kwa mtoto wako?

Baba mzazi wa taifa la Israeli Mungu analiita taifa la Israeli watoto wake (Kut 4:22). Mara nyingi anawalinganisha na watoto wasiotii. Hata hivyo Mungu ameendelea hadi leo kuwakumbatia na kuwavuta katika pendo lake. Hii haina maana hakuwapa adhabu walipomwasi, la hasha. Pale walipokosa waliadhibiwa, lakini daima lengo la Mungu ni kuwarudisha pendoni mwake. Hakuwahi kuwakatia tamaa na kuwaacha. Waliopotea ni wale tu walioendelea kukataa katakata kukaa katika wema wake (Rum 11:22).

Watoto wa Gen Z

Kuna watu wanaozaa bila utaratibu, lakini hakuna mtoto aliyezaliwa kwa bahati mbaya. Kila mtoto anayezaliwa katika ulimwengu huu anazaliwa kwa sababu ya Mungu. Na Mungu ataka watu wote wawe watoto wake (1 Tim 2:4). Katika kusudi hili la Mungu, wewe kama mzazi au mlezi wa mtoto unakuwa umeaminiwa na Mungu kumlea mtoto huyo ili amfahamu Mungu kama Baba yake na kuishi sawasawa na mapenzi mema ya Mungu. Unaweza usione hili kwa sababu ya utundu wa mtoto wako au changamoto

nyinginezo za malezi. Lakini je, nani ajuaye kesho ya huyo unayeona hasikii wala hatii mtu yeyote? Huyo huyo unayeona ana hali hiyo, Mungu anampenda na kuwa na mawazo ya amani naye wala si ya mabaya. Basi, hali ya sasa ya mtoto huyo isikufanye kukata tamaa ya kutimiza wajibu wako wa malezi.

Mungu asikia sauti ya kijana

Angalia mfano ufuatao na kuutafakari kwa makini:

Hajiri alimkatia tamaa kijana wake kwa sababu ya kukosa maji wakiwa jangwa la Beer-sheba: “Yale maji yakaisha katika kiriba, [Hajiri] akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia” (Mwa 21:15-16).

Mama huyu alikosa tumaini la kuweza kumsaidia mtoto wake. Kwa maoni yake hakukuwa na namna ya mtoto wake kuweza kuinuka tena. Amemkatia tamaa.

Lakini Mungu, je? Ni muhimu sana kuangalia namna Mungu anavyomtazama kijana huyu: “Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa” (Mwa 21:17-18).

Mungu anamtazama kijana huyu aliyeko katika hali ya kufa na kumhurumia. Ishmaeli aendelee kuishi. Kwa hiyo anamtia moyo mama yake kuondoka na

kumsaidia mtoto wake. Thamani ya mtoto mbele za Mungu ni kubwa mno. Huyo unayemkatia tamaa, kijana huyo huyo ana thamani kubwa sana machoni pa Mungu.

Mungu anamtaka aishi naye kama baba anavyoishi na mtoto mpendwa. Anataka kumpa maisha yenye furaha ya kutumikia mapenzi yake Mungu katika ulimwengu huu.

Mwulize Mungu jinsi ya kufanya

Badala ya kukubali changamoto hizi zinazokuchochea kukata tamaa, utafute kujenga tabia ya kumwuliza Mungu juu ya hali mbalimbali ngumu unazokutana nazo kwa mtoto wako. Rebeka alikutwa na changamoto aina hiyo wakati akiwa na ujauzito wa Esau na Yakobo.

Ilimfanya akate tamaa na kutamani kifo, kwa sababu “watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza Bwana” (Mwa 25:22). Hatua muhimu aliyoichukua Rebeka ni ku-

mwuliza Mungu kwa nini anapitia magumu hayo. Jibu la Mungu lilimpa Rebeka ustahimilivu juu ya hali ngumu aliyokuwa anaipitia (tazama Mwa 25:23).

Baadaye Rebeka alijaa uchungu kwa ajili ya chaguo la Esau la kuwaoa wanawake wawili wa kabila lisilomwamini Bwana (Mwa 26:34). Lakini tunasoma pia kwamba Rebeka aliendelea kujitahidi kumsaidia Yakobo ampate mke mwenye imani katika Mungu.

Usimkatie tamaa mtoto wako. Mungu alimtuma Mwanawe aende akamtafute yule aliyepotea. Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi, na kumrejesha nyumbani (Lk 15:3-7 na 19:10). Jitoe kadiri uwezavyo kuhakikisha ya kwamba unakuwa sehemu muhimu ya mtoto wako kufikia makusudi hayo ya Mungu katika maisha yake.

Mch. Morice Mapundi

Mafafanuzi ya Zaburi 23 na neno lake kuhusu kupita kati ya bonde la uvuli wa mauti

Soma Biblia Kila Siku 2025

Je, unatafuta kumtukuza Mungu kwa kumzalia matunda? Basi, maneno ya Yesu na yakae ndani yako.

Jipatie nakala ya mwongozo huu utakaokusaidia kujisomea Biblia kwa mpango kila siku mwaka mzima wa 2025 pamoja na maelezo mafupi ya kukusaidia kutafakari na kuelewa Neno ulilosoma.

Faraja kwa kila aliyefiwa na mpendwa wake

Turn static files into dynamic content formats.

Create a flipbook
Issuu converts static files into: digital portfolios, online yearbooks, online catalogs, digital photo albums and more. Sign up and create your flipbook.