
Septemba/2024 - Novemba/2024

Septemba/2024 - Novemba/2024
S.L.P. 2696, Arusha 0759 544 917
Barua pepe: editor.somabiblia@gmail.com
Kamati ya Riziki:
James Sabuni (mhariri)
Mch. Anza Amen Lema
Mch. Philip Bach-Svendsen
Cathbert Msemo
Mary Bura
Magreth Mushi
Mch. Gervas Meitamei Luhekelo Sanga
Waandishi walioshiriki:
Mch. Gideon Mumo
Flora Michael
Mch. Elitegemeo Y. Mpumpa
Mch. Oswald Ndelwa
Layout: Cathbert Msemo
Jalada: Cathbert Msemo
ISSN 2683 - 6491
Nakala: 5000
Usambazaji: SOMA BIBLIA
S.L.P. 2696, Arusha
S.L.P. 12772, Dar es Salaam
S.L.P. 1088, Iringa
S.L.P. 6097, Mwanza
S.L.P. 1062, Mbeya
S.L.P. 4231, Dodoma
www.somabiblia.or.tz
Neno la Injili kwa rika zote
Tanzania!
Imechapwa na: Imaging Smart Dar es Salaam
Mungu wetu anatupenda bila kujali tumeangukia mbali kiasi gani, na bila kujali tunawaza au kufanya mabaya kwa kiwango gani. Kama tunayo pumzi bado Mungu anaona uwezekano wa kuturudisha kwake. Yeremia anasema, “Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele: ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu” (Yer 31:3). Upendo wa Mungu ni mkuu kama unavyoshuhudiwa katika hamu yake na dhamira ya kwamba sisi tuishi naye milele.
Zaidi sana upendo wa Mungu umeshuhudiwa kwetu kwa njia ya tunu ya thamani ya Mwanawe pekee Yesu Kristo, ambaye alimtuma ili awaokoe wanadamu wote.
Mada kuu katika toleo hili la tatu la Riziki 2024 ni Mungu wa Agano. Tunakumbushana kuwa upendo wa Mungu kwa mwanadamu ni upendo wa kipekee ambao hauwezi kulinganishwa na upendo wa aina yoyote ile. Ahadi ya kwamba hatatuacha yafungamana na agano lake nasi. Kama tukitoka kwenye agano hilo, tumepoteza ahadi hiyo. Kwa njia ya agano, Mungu ametuweka kwenye mikono yake, na anatuangalia na kutulinda kila wakati tusipatwe na hatari yoyote.
Katika toleo hili utasoma habari za mtu mmoja ambaye Mungu alimwokoa yeye na jamaa yake. Kupitia mtu huyu, Mungu aliweka agano kwa ulimwengu akiahidi kuwa hataangamiza dunia tena kwa maji. Pia kuna makala na shuhuda nzuri za kujenga na kukukumbusha kuwa Mungu anakupenda, haijalishi hali yako ya sasa. Yeye katika neno lake anasema, ”Naam, hawa [akina mama] waweza kusahau [watoto wao wanyonyao], lakini mimi sitakusahau wewe” (Isa 49:15).
James Sabuni
Uk. 3-4: Ubatizo kama agano
Uk. 5: Nakuapia Yesu
Uk. 6-7: Nuhu na ishara ya upinde wa mvua
Uk. 8-9: Kama ajira hakuna, je, tukae tu?
Uk. 10-13: Agano jipya la Yesu Kristo
Uk. 14-15: Wajibu wetu katika uchaguzi
Kila Mkristo hubatizwa. Ubatizo huweza kufanywa kwa njia tofauti, yaani kwa unyunyiziwaji wa maji katika paji la uso au kuzamishwa ndani ya maji, lakini kwa vyovyote maana yake ni “kuingizwa rasmi katika imani ya dini ya Kikristo”.
Ubatizo ni mlango wa kuingia katika kanisa. Kwa hiyo si kitu kigeni kwetu.
Hata hivyo bado kuna haja ya kuchunguza zaidi Ubatizo ni nini hasa. Huu una uhusiano gani na kuingia kwenye Ufalme wa Mungu, na maana yake ni nini kwa maisha ya Kikristo?
Mfano wa gharika kuu Hata kabla ya Yesu kuzaliwa, Wayahudi waliwabatiza watu wa Mataifa waliotaka kujiunga na dini ya Kiyahudi, lakini lilikuwa jambo jipya Yohana alipoanza kuwabatiza Wayahudi waliotaka kumgeukia Mungu kwa upya na kujiandaa kwa kuja kwa Masihi.
Hata hivyo tunakuta mfano wa Ubatizo mapema sana katika Agano la Kale. Nuhu na familia yake waliokolewa kutoka kwenye gharika (Mwa 6-9). Akikumbusha yaliyotokea, Petro anasema kwamba “mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi” (1 Pet 3:21).
Gharika kuu ilikuwa hukumu ya Mungu kwa wanadamu (Mwa 7:21-23). Maji yake yalileta kifo, na dunia ya wakati ule iliangamia (2 Pet 3:6). Nuhu peke yake na jamaa yake ndio waliopata neema ya Bwana wakapona hukumu ile (Mwa 6:8).
Petro anaeleza kuwa maana ya maji ya Ubatizo “siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele
za Mungu” (1 Pet 3:21). Tafsiri nyingine iliyo sahihi ya maneno ya asili ni kwamba Ubatizo ni rehani au agano kuhusu dhamiri njema.
Habari hii yaonesha kuwa Ubatizo ni zaidi ya ishara ya tendo la utii katika kumfuata Kristo. Hufungamana na wokovu. Kuwasili kwa Kristo na hasa kufa na kufufuka kwake kulianzisha agano jipya, na wote wanaoingia katika agano hili na Mungu kwa njia ya Ubatizo na imani, wanapewa wokovu pamoja na dhamiri safi katika uhusiano wao na Mungu. Ufufuo wa Yesu huwatoa waamini kutoka katika hukumu ya kifo.
Katika Agano la Kale manabii walitumia maji kama ishara ya nje ya utakaso wa ndani (Isa 1:16; Eze 36:25; Zab 51:2). Vivyo hivyo maji ya Ubatizo ni ishara ya nje ya tendo la Mungu ndani yao wanaobatizwa. “Tulizikwa pamoja naye [Kristo Yesu] kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende kwa upya wa uzima” (Rum 6:4).
Kama vile dunia ya zamani ilivyoangamia kwenye gharika kuu, kiini cha Ubatizo ni kifo cha Yesu ambacho kinaondoa hali yetu ya dhambi na kusafisha mioyo yetu. Wakati huohuo, kama vile Nuhu na familia yake walivyokuwa salama ndani ya safina, Ubatizo unatuokoa kutoka kifo. Kiini chake ni kufufuka kwa Yesu. Kwa hiyo Ubatizo unatupa pia maisha mapya pamoja na Yesu tukimfuata kwa utii wa imani.
Ubatizo kama agano
Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili, “agano” ni ahadi ya utekelezaji wa jambo au ni makubaliano, maelewano, kiaga au mapatano.
Kupitia Ubatizo tunaingia katika agano na Mungu. Anaagana nasi kwamba yeye atakuwa Mwokozi na Bwana wetu, wakati sisi tutakuwa wana au watoto wake. Hivyo Ubatizo ni tukio muhimu na la msingi katika maisha yetu, kwa sababu hatuwezi kuingia Ufalme wa Mungu isipokuwa kwa kuzaliwa upya kwa maji na kwa Roho (Yn 3:8). Ubatizo ndio kuzaliwa huko katika Ufalme wa Mungu.
Kama rehani ya uhusiano huo mpya kati yetu na Mungu, yeye anatoa kipawa cha Roho Mtakatifu. Hiyo huoneshwa kwa ishara ya kuwekewa mikono na mtumishi wa Mungu wakati wa kubatizwa. Kuanzia hapo sisi ni mashahidi pamoja na Roho wa Mungu juu ya Yesu na matendo yake ya kutuokoa.
Kwa hiyo Ubatizo hufanyika katika jina la Utatu Mtakatifu, na tendo lake Mungu huyu katika maisha yetu hutuvuta kutii amri zake, ikiwa ni itikio la neema yake kwetu.
Ubatizo na msalaba
Mtu anapobatizwa, mchungaji humwekea alama ya msalaba usoni na kifuani. Kwa nini? Ili kujibu swali hili, tuangalie kwanza kwa kifupi maana ya msalaba.
Huenda ni Waajemi walioanza kuwasulubisha watu mnamo karne ya 6 k.K. Baadaye namna hii ya kuwaua watu ilitumiwa zaidi na Warumi. Mhalifu alifungwa au kupigiliwa misumari kwenye msalaba wa mbao na kuachwa hadi kufa. Kifo kilichotokana na mateso ya msalaba
kilikuwa kichungu na chenye maumivu makali.
Katika Biblia msalaba unamaanisha kifo na kuhusiana na hukumu ya Mungu. “Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti” (Gal 3:13). Lakini kwa sababu Yesu alifanywa laana kwa ajili yetu alipokufa msalabani, maana ya msalaba leo ni tofauti kabisa. Katika msalaba sisi tunakutana na upendo wa Mungu unaotuvuta kwake. Paulo anasema kwamba “neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaokolewa ni nguvu ya Mungu” (1 Kor 1:18-25).
Maisha mapya ya aliyebatizwa Yesu mwenyewe ndiye maana ya Ubatizo na nguvu yake. Rum 6:6 hueleza jinsi nguvu hiyo inavyoonekana katika maisha ya waliobatizwa. Kupitia Ubatizo “utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye [Kristo], ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena.” Kwa kuunganika naye katika mfano wa mauti yake, maisha ya kale ya aliyebatizwa yamepita. Ndivyo Ubatizo na msalaba vinavyofungamana.
Wakati huohuo yule anayebatizwa anapewa maisha mapya ya kumfuata Mwokozi wake kwa imani. Alama ya msalaba inamaanisha kwamba amenunuliwa kwa damu ya Yesu na ni mali yake.
Kuanzia sasa ni wajibu wake kumfuata
Bwana wake mpya. Akiwa chini ya ulinzi wake, aliyebatizwa ameitwa na kuwezeshwa na Mungu kuwaleta wengine kwa
Bwana Yesu kwa njia ya ushuhuda wa maneno na matendo kuhusu matendo ya Mungu ya kumpatia wokovu.
Mch. Gervas Meitamei
Tuko wengi tuliowahi kupitia ahadi, kiapo au maagano yaliyovunjika. Pengine ilikuwa marafiki zetu waliovunja ahadi yao, au sisi wenyewe tulifanya.
Jambo hili halihusu sisi kwa sisi tu. Watu wengi huweka agano kwa Mungu, hasa wanapokuwa na uhitaji mkubwa, kisha huacha kuzitimiza ahadi zao, hata nyakati zinapokuwa bora na kuwawezesha kuzitimiza. Je, ni kwa sababu gani?
Wengi humwambia Mungu, “Ukiniponya, au ukinisaidia kuepuka jambo hili, au ukinisaidia kupata kazi hii mpya, ukinisaidia kupata fedha ... nitafanya moja, mbili, tatu.” Lakini loooh! Mungu akiwapa, wanasahau agano walilofanya. Kuna wimbo mzuri unaoweza kutukumbusha umuhimu wa kutunza ahadi zetu kwa Mungu na kuzitimiza. Daima ni sisi tunaovunja agano. Mungu akifanya agano, siku zote anatimiza agano. Wimbo huo unaitwa Nakuapia Yesu. Ni wimbo namba 312 katika Tumwabudu Mungu
Wetu.
Mtunzi wa wimbo ni John Ernest Bode (1816-1874). Alihudumia kama kasisi wa Kianglikana katika parokia ndogo karibu na Cambridge, Uingereza. Alikuwa na watoto watatu, binti mmoja na wavulana wawili. John Bode aliwatungia wimbo huu maalumu kwa ajili ya sherehe ya kipaimara yao.
John Bode aliwaambia watoto wake, “Nimeandika wimbo huu uliojaa kweli zote muhimu ninazotaka mkumbuke.”
Mara moja anataja lililo jambo la kwanza kwake katika ubeti wa kwanza: Nakuapia Yesu kukutumikia. Alilenga kuwajenga watoto katika utumishi mwema kama jibu la urafiki mwema na Mungu.
Wimbo huu hutukumbusha kuzingatia ahadi tunazozitoa tuzitimize. Agano kwa Mungu latakiwa kutekelezwa, na John Bode alijua kuna upinzani mwingi. Kwa hiyo wimbo unatukumbusha kumwomba Yesu atulinde kutoka katika hatari na majaribu yanayoletwa na ulimwengu. Tunaimba katika ubeti ule wa pili, Dunia i karibu, Bwana unilinde na majaribu mengi yako pande zote. John Bode anakumbusha vilevile kwamba Yesu pia anatoa ahadi kwenye kipaimara, nayo ni kubwa. Hatatuacha kamwe tunapozikanyaga nyayo zake Yesu, bali atatufikisha kuishi pamoja naye katika utukufu wake. Waagana na wote wakufuatao, kwamba uliko wewe, nao watakuwa. Na Yesu ni tofauti na sisi wanadamu. Yu mwaminifu, na tunaweza kutegemea kuwa atimiza ahadi zake zote kwetu. Mtunzi anaonesha imani yake katika ubeti wa mwisho akimaliza wimbo kwa maombi haya, Ee Yesu Mwokozi, nichukue nikifa na kwako mbinguni. Huu ni wimbo mzuri sana. Unafaa kuimbwa nyakati zote, si kwenye kipaimara tu. Natumaini sote tunaweza kuvutwa na wimbo huu na kuuweka kama njia nzuri ya kutukumbusha maagano yetu na Mungu ili kuyatimiza.
Je, unapata wazo gani unapoona upinde wa mvua? Asili ya maumbile? Lebo au ishara ya kundi fulani? Au tendo la neema ya Mungu kwa wanadamu? Tuangalie isemavyo Biblia.
Wakati wa Nuhu uovu wa mwanadamu ulifikia kilele. Matendo, mawazo na hata nia za mioyo, vyote vilikuwa kinyume cha mapenzi ya Mungu (Mwa 6:45). Watu walikula na kunywa, wakaoa na kuolewa, lakini bila ya kumjali Mungu (Lk 17:26-27). Waliishi kama hakuna Mungu, na hali yao hii ilimfanya Mungu kughairi kwamba amemfanya mwanadamu (Mwa 6:6).
Matokeo ya uovu huu Mungu aliwaangamiza wanadamu kwa gharika ya kuifunika dunia yote iliyosababishwa na mvua ya siku arobaini, mchana na usiku (6:7,17; 7:20). Walikufa wote, wanadamu, ndege, wanyama na kila kitambaacho, isipokuwa Nuhu, mkewe, wanawe watatu na wake zao, na wanyama aliowahifadhi Nuhu kwenye safina pamoja naye, sawa na agizo la Mungu (6:19-20; 7:21).
Baada ya mwaka mzima Nuhu na wanawe walitoka nje ya safina na kupokelewa na dunia tofauti kabisa. Kama kipofu aonaye kwa mara ya kwanza, walikutana na madhari tofauti, utupu usioeleweka wala kuelezeka na ukimya uliowakumbusha kwamba majirani na marafiki zao waliangamia kwenye gharika.
Tunaokolewa kwa neema tu Hapo ndipo Nuhu alipotambua kwamba ni kwa neema ya Mungu tu ali-
pata kuokolewa, yeye na wanawe (6:8). Shukrani yake ilikuwa kumjengea Mungu madhabahu na kumtolea sadaka ya kuteketezwa (8:20).
Lakini hata baada ya sadaka hii Nuhu alibaki bila kuwa na uhakika wa gharika. Hakuwa na namna ya kuhakikisha kutokuwepo kwa uovu tena kwake wala kwa wanawe. Bila Mungu kuingilia hali yake, Nuhu na wanawe wangeishi kwa hofu wakitaraji kupatikana na gharika nyingine wakati wowote.
Tunamshukuru Mungu, kwani aliposikia harufu ya kumridhisha kutoka kwenye ile sadaka aliweka agano lake kwa Nuhu lililomhakikishia usalama wake na wanawe, na wanyama wote na vyote alivyoumba.
Maji hayataiharibu tena dunia
Kwanza Mungu aliahidi kutoiharibu nchi tena kwa maji akisema, “Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, …. Wala hakutakuwa gharika tena, baada ya hayo, kuiharibu nchi” (8:21a, 9:11).
Utatambua kwamba ahadi hii haiwategemei Nuhu na wanawe. Haikuwekwa kwa sababu Nuhu amekuwa mkamilifu! La hasha! Imewekwa kwa sababu “mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake” (8:21b). Iwe Nuhu, au wanawe, au kizazi cha leo, hofu ya kupata adhabu ya gharika imeondolewa.
Majira na nyakati zitaendelea!
Pili, Mungu aliahidi kwamba misimu itakuja kwa wakati wake na kudumu kwa vipindi vyake akisema, “Muda nchi
idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi, na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku havitakoma” (8:21-22).
Maana yake, ingawa wakati fulani tunashuhudia vipindi virefu zaidi vya mvua, au hari au baridi, Mungu ameviwekea kikomo kwa ajili yetu.
Tatu, Mungu aliahidi kwa kusema, “Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, … kila kitambaacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, ... Atakayemwaga damu ya mwandamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu” (9:2,3,6a). Hapa Mungu anaahidi kuwalinda Nuhu na wanawe dhidi wa wanadamu wenzao na wanyama, na kuwapa wanyama kuwa chakula chao.
Lengo la upinde wa mvua
Kama ilivyokuwa desturi ya wakati huo, agano hili liliunganishwa na ishara. Lengo la ishara hii lilikuwa kuthibitisha kwamba siku zote Mungu atatimiza ahadi yake na kumlinda Nuhu pamoja na wanawe na
freeimages.com
hata sisi. Ishara aliyoichagua Mungu ni upinde wa mvua unaotokea wakati wa mvua kunyesha.
Mungu akasema, “Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu nanyi, … Mimi nauweka upinde wangu winguni, … Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, nami nitakumbuka agano langu, … wala maji hayatakuwa gharika tena kuharibu wote wenye mwili” (9:12-15).
Hivyo, upinde wa mvua ni ishara ya agano la Mungu kwa Nuhu na kwetu leo kwamba Mungu hataharibu nchi kwa gharika tena. Ni ishara kwamba Mungu anatuvumilia hata tufikie toba (2 Pet 3:9; ling. Rum 2:4). Ni ishara kwamba mpango wa Mungu sio kutuangamiza, bali kutuokoa na mauti ya milele kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu (Yn 3:16-17).
Mch. Gideon Mumo
Mimi ni binti wa umri wa miaka 33. Wazazi wangu walinilea katika maadili mazuri ya kumcha na kumtegemea Mungu katika mambo yote. Walijitahidi kunisomesha hadi kufikia ngazi ya chuo. Nilihitimu chuo miaka 8 iliyopita nikiwa na digrii ya ualimu.
Kwa sababu ya upungufu wa ajira, mara tu baada ya kumaliza chuo nilianza kujitolea katika shule mbalimbali za sekondari nikiamini kuwa itakapotokea nafasi basi wataniajiri. Nilifanya hivyo kwa miaka 2 nikijitolea. Sikuwa napewa mshahara isipokuwa nauli tu ya kwenda na kurudi nyumbani.
“Kazi
Kadri siku zilivyozidi kwenda, nilijikuta sina furaha kwa sababu nilikuwa natumika sana lakini sipati ujira unaolingana na elimu yangu. Basi, niliamua kuacha kujitolea, kwa sababu niliona napoteza muda wangu bure. Hivyo nilikaa nyumbani kwa wazazi wangu tu.
niambia, ”Binti yangu, karibu uji wa ulezi.” Nikamjibu, “Asante, siku nyingine.”
Yule mama akapita akaenda zake.
ya mikono yetu utufanyie thabiti, naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.”
Kadri siku zilivyoenda nilijitambua kuwa ni mzigo kwa wazazi. Nimegeuka kuwa ombaomba kwa wazazi, maana nilikuwa naomba kila kitu ili nijikimu kama binti. Sijawahi kuwasikia wazazi wangu wakilalamika. Walinielewa hali yangu, na walikuwa wananisaidia kwa kadri wawezavyo. Lakini ndani yangu nilikuwa napata shida sana, na nilijiuliza nitaendelea kuwa tegemezi hadi lini.
Siku moja mama mmoja alipita maeneo ya nyumbani kwetu. Mama huyu alikuwa amebeba kapu lililojaa chupa za chai. Na alipofika mahali nilipokaa aka-
Siku ya pili nilikuwa natoka mjini, nikakutana na yule mama tena. Wakati huu alikuwa anahudumia vijana wa gereji iliyokuwa karibu na nyumbani kwetu Tabata. Nilisimama kwa muda kumwangalia akiwahudumia vijana kwa kuwauzia uji wa ulezi. Baada ya muda yule mama alinisogelea na kuniuliza kama nilikuwa nataka kununua uji. Kwa kweli sikuwa na mpango wa kununua, lakini niliamua kununua ili nijifunze kitu kutoka kwake. Nilimwuliza yule mama bei ya kikombe kimoja cha uji, akaniambia anauza kwa shilingi mia tano tu. Nilimpa mia tano, na akanipatia kikombe cha uji. Uji ule ulikuwa mtamu sana. Wakati wa kunywa nikaendelea kumwuliza mama yule kuhusu biashara yake na hali ya soko. Bila shida mama yule akaanza kuniambia kuwa hiyo biashara ameifanya kwa miaka mingi, na alikuwa anasomesha watoto wake kwa biashara hiyo.
Wakati akiendelea kunielimisha kuhusu biashara yake, nilianza kuvutwa na mimi kuingia katika biashara ya namna hiyo. Kwa wakati ule, na nikitambua hali halisi ya uchumi wangu, niliamua kuweka pembeni elimu yangu ya chuo kikuu na uzuri wangu kama binti, na nikaomba mama yule anifundishe kutengeneza uji ili na mimi niuze, angalau nipate fedha ya kujikimu.
Kwa bahati nzuri mama yule hakuwa mchoyo. Alikubali kunifundisha, na siyo alinifundisha tu namna ya kuandaa uji wa ulezi, pia alinifundisha hata kutengeneza uji wa mchele. Baada ya mimi kuhitimu darasa hili, alinielekeza maeneo ambayo ningeweza kupata wateja. Nilimwomba mama yangu mzazi anisaidie kununua chupa nne kubwa kwa ajili ya kuweka uji, ili niende kuuza. Kweli, mama alininunulia chupa kubwa zenye uwezo wa kuingia vikombe kumi vya uji.
Baada ya kupata chupa hizi, nikaanza biashara ya kuuza uji nikianza na mtaji wa shilingi 18,000. Nilikuwa nauzia uji Ilala
Boma, na hasa maeneo ya gereji ambako kuna vijana wengi wanaofanya kazi huko.
Nilianza kwa kupeleka uji asubuhi na mapema wakati wanaingia kazini, kisha nilirudi nyumbani na kuanza kutayarisha uji mwingine kwa ajili ya jioni wakati wakijiandaa kutoka. Siku ya kwanza niliuza uji wote na kupata faida ya shilingi 12,500. Baada ya kuona faida hii ambayo ilikuwa ni muujiza mkubwa kwangu, nikaanza rasmi biashara hii. Nilikuwa nazunguka mjini kwenye vijiwe na magereji kutafuta wateja.
Katika mwezi uliofuata nilijikuta nimepata faida katika kazi yangu. Hivyo niliamua kwenda kanisani kutoa fungu la kumi katika pato langu lililotoka katika biashara yangu. Sehemu hii ya kumi haikuwa kubwa, lakini niliitoa kwa imani kulingana na biashara yangu. Wakati wote nikiwa katika biashara yangu niliongozwa na Zaburi 90:17 isemayo, ”Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.”
Uaminifu wa Mungu ni mkuu. Siku baada ya siku niliona nikiingiza faida kidogo kidogo. Niliondokana na hali ya utegemezi kwa wazazi wangu. Ninapoandika ushuhuda huu, nina furaha ya kukuambia kwamba sasa nimefungua mgahawa. Asubuhi nauza chai na vitafunio, na mchana nauza vyakula mbalimbali kwa wateja wangu. Nina vijana 4 wanaonisaidia pale kwenye mgahawa wangu na ninamshukuru Mungu kwamba naendelea vizuri.
Leo ninapokutana na vijana wenzangu ambao wanazunguka mtaani kutafuta ajira, nina jambo la kuwafundisha. Wasomi ni wengi, na kila mmoja anasubiri ajira za serikali. Lakini ajira zipo kama utaondoa fikra za kuwa ajira ni lazima uajiriwe na shirika au serikali au mtu binafsi. Unaweza kujiajiri mwenyewe kama nilivyofanya mimi. Ongeza kujiamini na kujishusha kufanya kazi yoyote ya halali hata kama siyo ya elimu yako, ilimradi maisha yaende.
Kazi zipo ukiamua kuzitafuta. Ila usitafute kazi kwa kuweka digree yako mbele. Ukifanya hivyo hutazipata. Wenye digree ni wengi, ila wenye akili na maarifa ya kujitafutia ajira ni wachache.
Biblia yatuambia kuhusu maagano kadhaa ambayo Mungu ameyafanya tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Maagano hayo yana maana kubwa tunapotaka kuelewa ujumbe wa Biblia, kwa sababu uhusiano wetu na Mungu huamuliwa na maagano hayo.
Siku hizi neno hili agano halitumiki sana. Badala yake tunazungumza juu ya mkataba. Watu wengi huchanganya maana na matumizi ya maneno hayo. Kwa hiyo tuangalie kwanza yana maana gani.
Mkataba
Mkataba ni “makubaliano yanayotiwa katika maandishi kati ya pande mbili au zaidi ambayo yanatekelezwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria”. Kwa mfano tuko wengi tulio na mkataba wa kazi, ambao huwekea pande zote mbili, mwajiri na mwajiriwa, masharti mbalimbali. Tena na tena tunakuta kwamba kuna mikataba inayobadilishwa na kuvunjika kwa sababu haijatekelezwa, au imevunjwa moja kwa moja.
Kuna watu katika Biblia wanaofanya mikataba. Kwa mfano kuna wafalme waliolazimisha nchi ya jirani “kulipa kodi”. Mara nyingi yule mdogo katika mkataba wa aina hiyo alitafuta kuuvunja (2 Fal 17:3-4). Lakini pia kuna watu walioahidiana kwa sababu wanapendana, na ahadi au mkataba wa aina hii uliweza kuleta baraka hata kwa familia yao (ling. 1 Sam 18:3 na 2 Sam 9:7).
Agano
Agano hufanana na mkataba, lakini mara nyingi zipo pia tofauti mbalimbali, hasa
tunapoangalia maagano yaliyoasisiwa na Mungu. Wakati mkataba unaratibisha wajibu na marupurupu ya pande zote za mapatano, maagano ya Mungu hufanana zaidi na ahadi ambayo anaitoa kwa mtu au watu fulani. Ahadi hiyo hao wanatakiwa kuipokea kwa kumwamini Mungu. Hivyo watakuwa na uhusiano mwema naye, na wataendelea kupewa baraka zile alizowaahidia Mungu.
Maagano ya Mungu huweza kuvunjwa na mwanadamu, huyu akimwacha Mungu. Walakini maagano hudumu kwa namna fulani, kwa sababu Mungu ndiye mwaminifu kwa neno lake. Mtu akimrudia, Mungu ni mwenye haki na kuendelea kumtendea kama alivyoahidi.
Agano la Kale na Agano Jipya
Tutaangalia mifano mbalimbali ya maagano kati ya Mungu na mwanadamu. Lengo ni kuelewa zaidi agano jipya ambalo Mungu alilifanya nasi katika Kristo Yesu. Lakini kwanza tuseme kidogo zaidi kuhusu tunavyotumia neno “agano” siku hizi.
Twasema kwamba Biblia ina sehemu kuu mbili ambazo huitwa Agano la Kale na Agano Jipya. Maana ya majina haya ni maandiko yale ambayo kwa pamoja yanafanyiza Biblia. Kwa kawaida tunatumia herufi kubwa tunapoandika juu ya maandiko hayo, Agano la Kale likiwa maandiko yale yaliyoandikwa kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, wakati Agano Jipya ni maandiko yale yanayosimulia habari za maisha ya Yesu Kristo tangu kuzaliwa kwake hadi kufa na kufufuka kwake, na utendaji wa Mitume wake na Kanisa la kwanza.
Lakini mara nyingi tunayatumia maneno hayo kwa namna nyingine pia. Tunaliita agano lile alilolifanya Mungu na wana wa Israeli “agano la kale” ingawa jina zuri zaidi ni agano la Sinai. Vilevile tunazungumza juu ya “agano jipya”, tukimaanisha agano lile aliloasisi Yesu wakati alipokufa kwa ajili yetu.
Yesu mwenyewe alilitaja wakati wa kusherehekea Pasaka ya Kiyahudi kwa mara ya mwisho, hapo aliposema juu ya divai kwamba “hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi” (Mt 26:28).
Tunapozungumzia agano na si maandiko, inafaa kutumia herufi ndogo ili kuweka wazi kwamba tunamaanisha uhusiano wa Mungu na watu wake.
Agano la Mungu na Nuhu
Tunaweza kusema kwamba Mwa 2:16-17 ni agano la kwanza alilolifanya Mungu na mwanadamu. Adamu na Hawa walikuwa waishi na Mungu kwa kuliamini neno lake hilo wakiacha kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
Lakini mara ya kwanza tunapokuta neno “agano” katika Biblia ni pale Mungu anapomwambia Nuhu, “Nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe” (Mwa 6:18).
Tukichunguza zaidi tunaona agano hili ni sawa na ahadi ya Mungu. Sababu ya Mungu kuitoa siyo kwamba Nuhu aliistahili, maana imeandikwa kwamba “Nuhu akapata neema machoni pa Bwana” (Mwa 6:8). Tunaweza kusema hilo ni agano la upande mmoja, maana Mungu hakuweka masharti yoyote. Ilibidi tu Nuhu amwa-
mini Mungu, akifuata alivyoambiwa kuhusu ujenzi wa safina.
Tunaona pia sifa nyingine iliyo ya kawaida kwenye maagano ya Mungu: Anaunganisha ahadi yake na alama au ishara fulani. Katika agano lake na Nuhu ni upinde wa mvua. Tangu mwanzo maana ya upinde huu ilikuwa kutukumbusha juu ya uaminifu wa Mungu, kama alivyosema mwenyewe: “Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi” (Mwa 8:12-14).
Hadi leo Mungu amekumbuka agano hili kati yake na binadamu, kama alivyoahidi: “Nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili” (Mwa 9:15; taz. pia 8:21-22).
Agano la Mungu na Ibrahimu Wanadamu walipomwasi Mungu kwa kujenga mnara wa Babeli, alishika ahadi yake. Mungu hakulaani nchi kwa kuleta gharika nyingine, bali aliendeleza agano lake na nchi kwa kufanya agano lingine na Ibrahimu kwamba atabariki Mataifa yote kupitia mzao wake, yaani, Kristo (soma Mwa 12:1-3; 17:7, 19; 28:18; Gal 3:16).
Mungu aliamua kwamba agano hili pia litakuwa na alama au kitambulisho ambacho ni tohara (Mwa 17:10-14). Pamoja na alama hii kuwatambulisha wote walioingia katika agano, iliwakumbusha pia mambo mengine: Agano lilitakiwa kupokelewa kwa imani. Inaonekana kwa
jinsi Mungu alivyojiwekea masharti yote ya agano kwa kupita yeye peke yake kati ya vipande vya wanyama siku ile alipofanya agano na Ibrahimu (Mwa 15:6, 9-18; Gal 3:6-9).
Hivyo wanawake pia watahusika ingawa hawakutahiriwa. Vilevile watoto wa kiume wenye umri wa siku nane tu, yaani kabla hawajafanya lolote, waliweza kuingia. Agano la Mungu na Ibrahimu halikuwa na ubaguzi wowote, maana hata Mataifa yote wahusika nalo. Msingi wa agano sio ukoo wala jinsia, maana baraka za agano humtegemea mzao huyo ambaye Mungu aliahidi kumpa Ibrahimu. Mungu mwenyewe alitekeleza ahadi yake kwa jinsi alivyotenda katika Kristo (Gal 3:13-14).
Kwa kuwa Mungu ndiye aliyeanzisha agano hili, naye ni mwaminifu kwa neno lake, tunaendelea kuona kwamba Mungu asikia, kuona na kushiriki hali zote zinazomkabili watu wake wa agano: “Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo” (Kut 2:24).
Kama Mungu alivyowakomboa watu wake wakati huo kutoka katika utumwa wa Misri, alitukomboa sisi katika Kristo. Kwa hiyo agano jipya la Yesu ni tokeo la uaminifu wa Mungu kwa ahadi yake aliyompa Ibrahimu.
Agano la Sinai
Ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa imani, basi, tuelewe namna gani agano lile ambalo mara nyingi tunaliita agano la kale, yaani, agano la Siani? Si kwamba liliwawekea Waisraeli masharti? Ndiyo, hilo lilikuwa agano la pande zote mbili au agano la sheria. “Torati haikuja kwa
imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo” (Gal 3:12).
Kwa hiyo Waisraeli walijipatia nafasi ya kuishi na Mungu kwa matendo, na kujistahilisha kuitwa watu wa Mungu kwa kuzitimiza amri zake? Hapana. Wazo hili lilikuwa kosa kubwa la Kiyahudi. Walisahau msingi wa hali yao kama watu wa Mungu, ingawa Mungu aliwakumbusha kama jambo la kwanza kabla hajawapa Amri Kumi: “Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa” (Kut 20:1).
Agano la Sinai pamoja na amri zake zote linadhihirisha jinsi watu wa Mungu wakati ule walivyotakiwa kuishi naye, lakini halikukusudia kuwa njia ya wokovu. Jambo hili limefafanuliwa wazi na Paulo katika Gal 3:17-18: “Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi.”
Soma mwenyewe Gal 3:19-29 juu ya kazi ya sheria au lengo lake kuu kabla hujaendelea kusoma hapa chini juu ya agano jipya!
Agano jipya
Agano la Mungu na Israeli kwenye mlima wa Sinai lilionekana kuwa dhaifu kwa jinsi watu wake walivyoendelea kulivunja. Lakini Mungu ndiye mwaminifu kwa neno lake na kutaka kuokoa na kubariki watu wake. Kwa hiyo alitangaza mapema jinsi atakavyoboresha uhusiano wake na watu wake ili kuhakikisha kwamba malengo yake yatatimia.
Kuanzishwa kwa agano jipya ni jibu lake. Ndivyo Mungu anavyoeleza bayana katika Yer 31:31-32: “Angalia siku zinakuja, asema BWANA, nitakakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri ambapo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao asema Bwana”.
Bila agano jipya hakuna maisha wala wokovu. Kinacholifanya kuwa bora ni kwamba limejengwa juu ya tendo la Mungu mwenyewe katika Kristo, na kwamba hataandika tena mapenzi yake kwenye mbao za sheria bali “ndani yao, na katika mioyo yao” walio watu wake.
Hivyo wanaolipokea agano hili jipya wanalipokea kwa imani. Lengo la agano jipya la Kristo Yesu ni kwamba wanadamu wote wamjue Mungu “tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao”, na watamjua kama Mungu anayeusamehe uovu wao (Yer 31:33-34). Msamaha huu ndio utaleta mabadiliko hayo ya ndani yao yatakayohakikisha kwamba watampenda Mungu na kuendelea kuishi naye.
Mdhamini wa agano jipya
Hakuna agano kuu kuliko agano hilo jipya. Sababu ni mdhamini wake ambaye ni Yesu Kristo. Ndiye “mjumbe wa agano jipya” kwa njia ya “damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili” (Ebr 12:24).
Yeye pekee aliliasisi agano hili kwa njia ya kifo chake msalabani. Anaeleza mwenyewe kwamba damu yake ni ya agano, na kumwagika kwake kutaleta ondoleo
hilo la dhambi lililo la lazima ili sisi tuweze kuishi na Mungu. Ndivyo tunavyokumbushwa kila mara tunaposhiriki Ushirika Mtakatifu. Huu ni chakula cha agano, kama vile pia agano la Sinai lilivyokuwa na mlo wa agano (Kut 24:9-11). Kwenye meza ya Bwana watu wa Mungu hukusanyika ili kusherehekea na kufurahia uhusiano wao mwema na Mungu, na kuimarishwa kiimani (Mt 26:27-28). Kwa hiyo Yesu Kristo ameagiza chakula chake cha agano kifanyike mara kwa mara.
Agano jipya linahusu upatanisho kati ya Mungu na watu wa kila rika, jinsia, taifa, kabila na rangi. Halina ubaguzi, kila mmoja anaitwa kukutana na Bwana na Mwokozi wake ili apokee msamaha wake na kuishi naye kwa amani (Rum 11:27). Kwa njia hii, Mungu ameingia katika mahusiano mapya na ya kipekee na mwanadamu.
Hakuna sharti la kujistahilisha kuingia katika agano hili jipya, maana Yesu Kristo ndiye utimilifu wake. Njia ya kuingia ni Ubatizo wa Kikristo. Inaonekana kwa mfano katika Kol 2:11-13. Akilinganisha agano jipya na agano la Sinai, Paulo anauita ubatizo “tohara ya Kristo”. Maana yake ni kuzikwa pamoja na Yesu katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye katika huo kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua Yesu katika wafu. Kila aliyebatizwa na kumwamini Yesu Kristo ni wa familia ya Mungu na kustahili kushiriki Meza ya Bwana.
Jamii yoyote ile ya mwanadamu ina viongozi wake, ila kihistoria kuna tofauti ya jinsi watu hawa walivyopata kuongoza jamii. Hadi leo si jamii zote zinazowapa raia nafasi ya kuchagua viongozi wake. Tutaangalia kwa ufupi jinsi mfumo wa uchaguzi wa viongozi katika nchi yetu unavyompa kila raia wajibu na fursa fulani.
Tumshukuru Mungu kutupa nchi iliyojengwa katika misingi ya amani na kwa jinsi inavyowapa raia wake kushiriki uchaguzi wa viongozi wake. Bila kujali tofauti zetu za kidini, kikabila na kisiasa, tuna nafasi ya kutoa maoni yetu kwa njia ya kupiga kura. Ni wajibu wetu wa msingi kutumia haki yetu hiyo ya kikatiba na kiraia ili tuchangie kujenga mustakabali bora wa pamoja kwa nchi yetu.
Kihistoria kumekuwa na changamoto na malalamiko katika baadhi ya nchi wakati wa uchaguzi na hata baada ya huo kufanyika, kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki. Njia tuliyo nayo sisi sote ya kuzuia isiwe hivyo katika nchi yetu ni kwanza kuombea jambo hili kwa Mungu, na kisha kushiriki kwa nia nzuri katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Katika maandiko matakatifu ya Biblia tunajifunza kuhusu umuhimu wa kutekeleza wito wetu huo wa kijamii wa kushirikiana kwa amani katika ujenzi wa nchi yetu.
Kupiga, kujipigia na kupigiwa kura
Katika Mithali 11:14 tunasoma kwamba “pasipo mashauri taifa huanguka; bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.” Nchi
yenye demokrasia hujali neno hili kwa kuwapa raia wote nafasi ya kupiga, kujipiga na kupigiwa kura. Kura huruhusu sauti zetu kuwa sehemu ya uamuzi wa pamoja, na kama tukitumia nafasi yetu vizuri, mfumo huu hutusaidia kupata viongozi wanaofuata kanuni za haki na hekima.
Umuhimu wa kuelimishana
Uchaguzi wa viongozi wa jamii kwa njia ya kupiga kura hutegemea mambo fulani ya msingi ili ufanikiwe vema.
Nabii Hosea alilia kwa sababu, kama ilivyoandikwa katika Hos 4:6, “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.” Maana yake kwa uchaguzi ni kwamba ni muhimu kuelimishana kuhusu sera na wagombea ili mpiga kura kufanya maamuzi ya busara. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kujielimisha na kuelimishana juu ya mambo hayo, lakini viongozi wa nchi wana wajibu wa pekee wa kuzingatia maarifa ya raia kwa kuwaelimisha kuhusu mambo yote ya uchaguzi.
Kuheshimu maoni ya wengine
Jambo lingine tunalokumbushwa na Biblia linapatikana kwa mfano katika Rum 12:18: “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.”
Amani hii hutegemea kuheshimu maoni ya wengine. Tunapowathamani wenzetu kwa kuwapa nafasi ya kutoa maoni yao na kushirikiana nao kwa upendo, tunajenga jamii imara na yenye amani inayokidhi mahitaji ya raia wote.
Yesu anawaambia wanafunzi wake, “Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Uzoefu wetu wa kupatanishwa na Mungu tunaweza kuutumia pia wakati unapohitajika upatanisho kati ya watu na hata kati ya vyama vya siasa.
Kuwahimiza viongozi
Hatimaye mustakabali bora wa pamoja kwa nchi yetu hutegemea kwamba tunaheshimu matokeo ya uchaguzi. Ni jukumu letu kama raia na waumini.
Waliochaguliwa kuwa viongozi wa jamii wanahitaji kwamba tunawajibika kwa kushika sheria wanazoziamua. Ikiwa tutaona kuna sheria isiyofaa, njia siyo ku-
lalamika tu wala kuivunja, bali kuchangia kwa maendeleo ya nchi kwa kushirikisha maoni yetu kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu na kuwapa raia wote haki yao.
Biblia ni wazi katika jambo hili: “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu ... Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu” (Rum 13:1nk).
Tunapaswa kuwaombea viongozi wetu na kuwahimiza kufanya kazi nzuri kwa niaba yetu na kutekeleza ahadi zao kwa uwazi na uwajibikaji. Tunaweza kufanya hivyo kwa kushiriki katika mijadala ya umma na kufuatilia utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo kwa ajili ya maslahi ya umma.
Kwa kuhitimisha, wajibu wetu wa kupiga kura katika uchaguzi ni muhimu kwa kujenga mustakabali bora katika nchi yetu. Sisi wenyewe tuwe wa kwanza wa kuwajibika kwa uadilifu. Hivyo tunamsifu Bwana wetu tunayemwamini na kuwa baraka kwa nchi yetu.
Agano la milele
Kuwepo kwa agano jipya kunafanya agano hilo lingine alilolifanya Mungu na wana wa Israeli kukaribia kwisha, kama ilivyoandikwa katika Ebr 8:13, “Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.”
Maana yake siyo kwamba Mungu amelivunja la awali, bali ameliweka lingine lililo bora zaidi. Agano jipya ni tofauti kabisa na lile la zamani. Lina kibali, utendaji na muhuri wa Yesu Kristo mwenyewe. Kwa hiyo ni agano la milele (Ebr 13:20). Litadumu hadi Yesu Kristo arudipo ku-
anavyofanya agano na sisi, na kudumisha uhusiano mwema wa agano kati yake na sisi. ... kutoka uk. 13
lichukua Kanisa ili kuishi pamoja milele katika ufalme wake wa utukufu.
Kwa mantiki hii, kuanzia kufufuka na kupaa kwa Yesu Kristo, Mungu hasemi na watu kwa njia nyingine isipokuwa Yesu Kristo tu (Ebr 1:2). Agano jipya linatualika sisi sote kuishi maisha mapya na Mwokozi wa ulimwengu. Wito wetu ni kulisikia, kulipokea, kuliamini na kuliishi agano hili. Njia mojawapo ni kushiriki Meza ya Bwana, “maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” katika utukufu wake (1 Kor 11:26).
Mch. Oswald Ndelwa & Philip Bach-Svendsen
Soma zaidi juu ya Mungu