Mfalme, makuhani, wakuu wa serikali, wote walilazimika kutii na kufuata amri za watu waliochafuka mawazoni na kuwa kama wenda wazimu. Wale waliotangaza kifo cha mfalme walimfuata pia kwa kumnyonga. Machinjano yalikuwa mengi sana. Watu wote wliodhaniwa kuwa hawayaungi mkono mapinduzi walichinjwa ovyo. Ufaransa ikawa mbuga ya majeshi ya watu wasio na utaratibu, wakizunguka zunguka na kuchijana. Katika mji wa Paris machafuko yalikuwa yakifuatana mfululizo, na raia waligawanyika katika vikundi vya usaliti; visivyokuwa na jambo la kufanya ila kuzungukazunguka tu na kufanya ghasia. Nchi ilikuwa karibu kufilisika, jeshi la askari ililikuwa likifanya ghasia, likidai mishahara ya nyuma ambayo haikulipwa. Watu katika mitaa walikuwa shidani kukosa chakula, mikoani kulijaa maharamia ambao walipora kila kitu kilichoonekana, na ustaarabu ulikuwa katika ukingo wa kutoweka kwa ajili ya fujo na ghasia zilizoenea kila mahali bila mtu wa kuzikomesha. Kengele iliyopigwa usiku wa manane ndiyo iliyokuwa alama ya machinjo yake.