RIZIKI TOLEO 1/2023 - Kuishi maisha ya ushuhuda

Page 1

RIZIKI

Machi/2023 - Mei/2023
1/2023
KUISHI MAISHA YA USHUHUDA TOLEO LA

RIZIKI

S.L.P. 2696, Arusha

0759 544 917

Barua pepe: editor.somabiblia@gmail.com

Kamati ya Riziki:

James Sabuni (mhariri)

Mch. Anza Amen Lema

Mch. Philip Bach-Svendsen

Cathbert Msemo

Mary Bura

Magreth Mushi

Mch. Gervas Meitamei

Luhekelo Sanga

Waandishi walioshiriki:

Mch. Gideon Mumo

Senteu Marwa

Layout: Cathbert Msemo

Jalada: Cathbert Msemo

ISSN 2683 - 6491

Nakala: 5000

Usambazaji:

SOMA BIBLIA

S.L.P. 2696, Arusha

S.L.P. 12772, Dar es Salaam

S.L.P. 1088, Iringa

S.L.P. 6097, Mwanza

S.L.P. 1062, Mbeya

S.L.P. 4231, Dodoma

www.somabiblia.or.tz

Neno la Injili

kwa rika zote

Tanzania!

Imechapwa na:

Imaging Smart Dar es Salaam

MADA TAHARIRI Kila mtu ana mshuhuda

Kuishi maisha ya ushuhuda

Wakristo hatuna hadithi mmoja tu, bali tunazo hadithi nyingi za matendo makuu ya Mungu. Ushuhuda wetu ni hadithi za nguvu na uwezo wa Mungu katika maisha yetu. Kila siku mpya katika maisha yetu huleta hadithi mpya za wema na neema ya Mungu. Hivyo ni sawa kusema kwamba

kila mkristo ana hadithi binafsi ya kusimulia, hasa tunapokumbuka kuwa Mungu ametuita mahususi, kama watu

maalum na muhimu. Hadithi ya maisha yako ni ushuhuda

wa wema wa Mungu, neema yake, na msamaha wake.

Katika toleo hili la Riziki tunajadili kichwa kisemacho, “Kuishi maisha ya ushuhuda’’. Lengo ni kukumbushana

kuwa kila mmoja wetu anayo hadithi ya kushuhudia. Hadithi yako kuhusu kutembea na Kristo au changamoto

ulizokutana nazo maishani zinaweza kufundisha, kujenga na kubadilisha maisha ya mtu mwingine anayepita kwenye hali kama yako.

Ndani ya toleo hili la Riziki utakutana na kijana mmoja

ambaye hadithi yake haisemwi sana, lakini kidogo alichotuachia kina maana kubwa sana. Kijana huyu aligundua kuwa mchumba wake ni mjamzito. Sheria ya kwao ilikuwa wazi kuwa mwanamke aliyefanya jambo kama hilo alistahili adhabu kali. Lakini kijana huyu aliazimia tofauti. Unataka kujua kilichotokea? Fungua usome!

Pia utakutana na mada mbalimbali na shuhuda zitakazokusogeza mbele katika maisha yako ya kutembea na Kristo. Nami nasema, “Shuhuda zako, [Bwana], nimezifanya urithi wa milele; maana ndizo changamko la moyo wangu” (Zab 119:111).

Yaliyomo:

Uk. 3-4: Kuishi maisha ya ushuhuda

Uk. 5-7: Mtoto ni mali ya nani?

Uk. 8-9: Yusufu

Uk. 10-11: Upendo wa familia ulinivuta kwa Yesu

Uk. 12-13: Kuitangaza mauti ya Bwana hata ajapo

Uk. 14-15: Ibada huanzia nyumbani

“Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya” (Lk 24:48). Ndivyo Yesu alivyowaambia wanafunzi wake mara kabla ya kuagana nao, akiwakumbusha juu ya kufa na kufufuka kwake mwenyewe. Hiyo inaonyesha kwamba ushuhuda wa kikristo unamhusu Yesu na matendo yake makuu ya wokovu. Habari zinazotangulia katika Luka 24 zinatuambia kwamba ni ushuhuda ulio na asili mbili: Wanafunzi walikuwa wameona na kusikia

wenyewe mambo hayo wakiongozana na Yesu (m.39; ling Mdo 1:21-22), na Yesu

alikuwa amewafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko (m.45).

Walengwa wa ushuhuda huo ni mataifa yote, na lengo lenyewe ni kwamba wapatanishwe na Mungu kwa njia ya kutubu na kupokea ondoleo la dhambi kwa jina la Yesu (m.47). Kwa maneno mengine, Yesu anataka watu wote wawe wanafunzi wake.

“Watahubiriwa”, Yesu anaeleza (m.47), na ndivyo waliopokea agizo lake kama wa kwanza walivyofanya. Tukumbuke kwa

mfano mahubiri ya Petro siku ya Pentekoste. Angalia kwamba imeandikwa katika Mdo 2:40 kuwa Petro “akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana”.

Kwa maneno na maisha!

Lakini ushuhuda wa kikristo ni zaidi ya maneno. Ni maisha ya ushuhuda, yaani matendo yetu yaambatane na maneno

yetu, na yote yamshuhudie Mwokozi na

Bwana wetu ili wasiomwamini wavutwe na kuongozwe kwake. Petro mwenyewe ni wa kwanza kulikumbusha jambo hili: “Mwe na mwenendo mzuri kati ya

Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa” (1 Pet 2:12; ling. 3:1nk).

Neno hili la mwisho linatuambia kwamba wasioamini hao wanaopata kuona matendo yetu mazuri, wataokolewa Mungu akipenda, na pamoja na maneno yetu Roho Mtakatifu atatumia pia matendo yetu ili kuwahakikishia kuwa Yesu ndiye Mwokozi wao pia.

Mfano wa Yohana Mbatizaji

Tutachukua mifano mitatu katika Biblia ili kujifunza zaidi maana ya kuishi maisha ya ushuhuda. Mtu wa kwanza ni Yohana mbatizaji. “Huyo alikuja kwa ushuhuda”, yaani maana ya maisha yake yote ilikuwa kumshuhudia Yesu ili “wote wapate kuamini” (Yn 1:7).

Kwa kweli maneno ya Yohana yaliwavuta watu kwa Yesu. Hata wanafunzi wa Yohana walimwacha ili kumfuata Yesu (Yn 1:29, 35-37). Hapo Yohana alitoa pia ushuhuda mkubwa kwa maisha yake akikubali kupungua yeye ili Yesu azidi (Yn 3:30).

Siri ya ushuhuda wa Yohana ilikuwa kwamba alishikamana na neno la Mungu na kuliona kuwa na thamani kubwa kuliko maisha yake mwenyewe. Hivyo alikuwa tayari kuteseka, Herode alipomfunga gerezani kwa sababu hakutaka kutubu alivyomchukua mke wa mtu mwingine na kukaa naye (Mt 14:3nk).

Tunaona pia kwamba siyo lazima maisha yetu yawe na mafanikio ili kumshuhudia Yesu. Siyo lazima kusubiri mpaka

3 2 RIZIKI TOLEO 1, 2023 RIZIKI TOLEO 1, 2023
James Sabuni

hali yetu ikae sawa tena. Hata Yohana alipokuwa gerezani na kupata wasiwasi

kama kweli Yesu alikuwa Masihi, aliwapeleka wanafunzi wake kwa Yesu (Mt 11:2nk)!

Mfano wa mwanamke wa Samaria

Mfano mwingine ni yule mwanamke wa Samaria. Kwa kweli maisha yake hayakuwa ushuhuda mzuri. Yawezekana alikwenda kuchota maji saa sita kwenye jua kali ili kuepuka jinsi wengine walivyozungumza maneno ya kudharau juu ya uhusiano wake na wanaume.

Lakini huyo mwanamke alipomkuta

Yesu kisimani, na Yesu alimsaidia kwa upendo kuona kwamba Yesu ni Masihi, habari hiyo njema inakuwa kama maji yaliyo hai yanayombubujikia uzima wa milele. Mara moja yule mwanamke anauacha mtungi wake na kukimbilia

mjini ili kumshuhudia Yesu.

Zingatia mambo mawili kuhusu ushuhuda wake (taz. Yn 4:29): Kwanza, anamtambulisha Yesu kama mtu aliyemwambia mambo yote aliyoyatenda.

Hana la kuficha tena kuhusu maisha yake. Ni kana kwamba aibu yote imekwisha, kwa sababu amemkuta mtu anayempenda, na huyu mtu amempa maisha mapya. Pili, ushuhuda wake hauna maneno mengi wala hawezi kueleza mengi. Anauliza swali tu, na kusema, “Njoni, mtazame”.

Licha ya ushuhuda wake huo kuwasaidia Wasamaria wengi kumwona Yesu na kumwamini, unatutia moyo sisi pia kumshuhudia Yesu. Hata kama maisha yetu yamefeli namna gani kama maisha yake mwanamke huyo, yanaweza kuwa

ushuhuda juu ya Yesu. Maana amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea, sivyo! Na ule upungufu katika ushuhuda wetu, Yesu anaufidia. Soma Yn 4:42!

Wenye barua ya Kristo mioyoni

Mfano wa mwisho ni Paulo. Si ushuhuda wa maisha yake mwenyewe, ingawa ni mkubwa, bali jinsi alivyoandika kuhusu maisha ya Wakristo wa Korintho kuwa ushuhuda.

Anawakumbusha kuwa maisha yao ni kama barua kutoka kwa Kristo Yesu ili isomwe na watu wote. Paulo hana haja ya uthibitisho mwingine kwamba yeye ni Mtume wa Kristo, kwa sababu “mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama” (2 Kor 3:34).

Hata hapo Korintho siri haikuwa kwamba maisha ya Wakristo yalikuwa ya ajabu yenye nidhamu ya juu na mafanikio mengi kwa mtazamo wa kibinadamu. Tukisoma barua za Paulo kwao, tunaona matatizo mengi ya kimaadili. Hata hivyo maisha yao yanaweza kuwa ushuhuda, kwa sababu ndio “waliotakaswa katika Kristo Yesu” (1 Kor 1:2). Pamoja na upungufu wa maisha yao wenyewe, walidhihirisha wema, uaminifu na neema ya Mungu.

Tumwombe Mungu kwamba Roho

Mtakatifu aandike neno la Kristo vivyo

hivyo mioyoni mwetu ili maisha yetu yote yamshuhudia Yesu kama Mwokozi na Bwana wetu.

Mtoto ni mali ya nani?

Tutafakari kwanza maana ya neno “mali”. Linatumika kuhusu kitu chochote chenye thamani ambacho kinamilikiwa na mtu. Ardhi, nyumba, magari na vitu vinginevyo ni mifano ya mali. Alama moja ya vitu hivyo ni kwamba huweza kuthaminishwa kwa fedha.

Biblia inasema kwamba “dunia ni mali ya BWANA, na vyote vilivyomo ndani yake” (Zab 24:1). Vyote hivyo ni pamoja na ”wote waishio ndani yake” dunia (Zab 24:1). Haijalishi kama ni mtoto au mtu mzima, sisi sote ni mali yake Mungu, maana ametuumba naye anaendelea kutupa uhai. Bila Yeye hatupo tena (Zab 104:29-30).

Mtoto ni wa Mungu

Katika Yeremia 1:5 Mungu anamwambia Yeremia, “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.” Daudi anashuhudia

vivyo hivyo katika Zab 139:13-16.

Hii inamaanisha kuwa licha ya kuwa asili ya mwanadamu na Muumbaji wa kila mtoto, Mungu ndiye pia anayemjalia mahitaji yote, kuongoza maisha yake na kumlea ili akue na kufikia makusudi ya Mungu kumleta duniani. Lengo kuu ni kwamba awe mwana wa Mungu anayeishi na Muumbaji wake kama mtoto aishivyo na baba yake mzazi (ling. Adamu anavyotambulishwa katika Lk 3:38).

Hiyo inatufundisha jambo muhimu na la msingi linaloweza kutusaidia kujibu swali la makala hii. Mtoto ni zaidi ya kitu kilicho mali ya mtu. Ni kiumbe hai aliye na thamani isiyoweza kulinganishwa na kiasi chochote cha fedha.

Amri hii, “Usiue” (Kut 20:13) hukaza jambo hili kwa namna yake. Uhai wa mtu ni mali ya Mungu. Hiyo pia ni sababu ya Wakristo kukataa kutoa mimba. Mimba siyo sehemu ya mwili wa mwanamke wala mali ya wazazi, bali Mungu amewaweka

5 4
RIZIKI TOLEO 1, 2023 RIZIKI TOLEO 1, 2023 MADA JAMII
Picha:Cathbert Msemo Mch. Philip Bach-Svendsen

kumtunza na kumpenda huyu mtoto na kumleta kwa Muumbaji wake aliyempa uhai.

Wazazi ni wakilishi wa Mungu Jibu la msingi kwa swali kuhusu mtoto ni mali ya nani, linapatikana katika amri nyingine ya Mungu, yaani, “Waheshimu baba yako na mama yako” (Kut 20:12).

Wazazi ni wakilishi wa kwanza wa Mungu katika maisha ya mtoto. Wamekuwepo

tangu huyu alipochukuliwa mimba na kutakiwa kuwa karibu naye muda wote wa utoto wake.

Hili linadhihirishwa hata na maneno yenyewe tunayotumia. Kwa mfano, Zaburi 127:3 inaposema, “Wana ni urithi utokao kwa BWANA, watoto ni zawadi kutoka kwake”, ni wazi kabisa kwamba wanaotunukiwa ndio wazazi.

Mungu mwenyewe ndiye aliyewapa haki na wajibu wa kumlea mtoto waliyemzaa. Kusudi lake ni kwamba mtoto ajitambue kama mtoto wa Mungu kupitia upendo wa wazazi wake, na kujifunza kumcha Mungu kwa njia ya kuwatii na kuwaheshimu wazazi.

Mtoto ni mali ya jamii nzima?

Siyo wote wanaotaka kuwapa wazazi kipaumbele hicho. Huona mtoto ni mali ya jamii. Mfano hasa ni falsafa ya Ukomunisti, lakini vilevile siyo wazo geni katika utamaduni wa Kiafrika. Hoja inayotolewa inaweza kujengwa ifuatavyo:

“Mungu aliitoa zawadi hii ya watoto kwa dunia, yaani watu wote au jamii, kwa ajili ya kuiendeleza na kuikuza dunia. Maana kutoka katika hali ya utoto ndimo chanzo cha kupata rasilimali watu

watakaonufaisha jamii ya watu kwa njia ya kuandaa dunia nzuri ya kesho na kuizalisha mali.

Tena ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha kwamba mali hii ya watoto watapata mahitaji yao, ili tuwe na jamii bora. Kuwatunza watoto ni kujitunza sisi wenyewe.”

Angalia maneno yanayotumika. Ni maneno kama “rasilimali”, “kunufaisha” na “kuizalisha mali”. Maoni hayo yanawageuza watoto walio viumbe hai vya Mungu kuwa “mali” - au hata “nguvukazi” tu katika falsafa ya Ukomunisti.

Jamii yahusika kama wa pili

Maneno hayo yenyewe huonyesha kwamba ni vigumu kupatanisha maoni ya mtoto kuwa mali ya jamii na mafundisho ya Biblia yanayosema wazi kwamba wazazi ni kwanza katika maisha yake. Lakini

hiyo haimaanishi kwamba jamii haihusiki na malezi ya mtoto wala kwamba walezi

hawawezi kumwasili mtoto ambaye hawajamzaa.

Ni kukaza tu kwamba kama vile walezi wanavyoingia mahali pa wazazi na kuwasaidia pale ambapo hao wameshindwa

kumlea mtoto wao, vivyo hivyo ni wajibu mkubwa wa jamii kuwapa wazazi

nafasi ya kuwalea watoto wao na hivyo

kuwawezesha kutimiza wajibu wao waliopewa na Mungu.

Jamii inaweza kuhakikisha mazingira

mazuri kwa malezi ya watoto, lakini

haiwezi kuwapa watoto ule upendo na uhusiano wa karibu ambao wazazi wa-

naweza, na ambao watoto huhitaji kuliko mambo mengine yote.

Ndoa na familia yenye wazazi na watoto wale waliojaliwa na Mungu ni taasi-

si ya msingi katika jamii. Jamii njema hutegemea familia imara ambapo watoto wanaweza kustawi na kupewa malezi bora. Jamii nzima - maana yake, sisi sote tulio watu wazima, tunao wajibu hapo kutegemeana na nafasi tuliyo nayo katika jamii na tuna uhusiano gani na familia ya watoto.

Kwa bahati mbaya kuna mifano si michache kwamba inabidi jamii kutumia mamlaka ile iliyo haki yake ya kuingilia kati na kumchukua mtoto asikae na wazazi wake, hao wanapomtunza vibaya na hata kuhatarisha maisha yake. Lakini jamii inayoheshimu mapenzi ya Mungu kuhusu malezi ya watoto, daima itajitahidi kama jambo la kwanza kuwasaidia wazazi kutengeneza hali ya kifamilia ili waendelee kukaa na watoto wao.

Tuwaombee watoto wetu Baba yetu wa mbinguni atujalie kutambua thamani ya mtoto ili tusimfanye kuwa mali tu tunayoweza kufaidika nayo. Kwanza na hata mwisho ndiye mtoto wa Mungu.

Atujalie pia kutambua kwamba wajibu wetu wa kwanza kama wazazi ni kumwakilisha Mungu vema ili mtoto apate kumtambua Mungu kama Baba yake mpendwa kupitia malezi yetu. Malezi mazuri ya watoto wetu ni namna ya kwanza ambayo kwayo tunaweza kutumikia jamii yetu.

Na Muumbaji wa mbingu na dunia awajalie viongozi wa jamii kutambua maana ya wazazi kwa mtoto ili wawekeze katika kuimarisha familia na kuwapatia wazazi nafasi nzuri ya kuwalea watoto wao. Bila shaka baraka za Mungu zitaonekana.

Mch. Philip Bach-Svendsen

7 6 RIZIKI TOLEO 1, 2023 RIZIKI TOLEO 1, 2023 JAMII JAMII
Picha: www.pixabay.com

Yusufu: Kijana aliyeishi maisha ya ushuhuda

Ni rahisi sana kupamba ushuhuda wetu kwa maneno, misemo na hisia ili kudhihirisha jinsi tunavyotembea na Mungu kwa karibu. Lakini ushuhuda wa kweli kwamba tunatembea na Kristo unapimwa hasa na utayari wetu wa kujinyima, kulipia, au hata kuteseka kwa ajili ya imani hiyo. Kwa mfano, siyo mengi yanayosemwa kuhusu Yusufu, mume wa Mariamu, mama yake Yesu. Lakini kidogo kilichosemwa juu yake kimetuachia ushuhuda wa kuigwa.

Kijana Yusufu alikuwa amemposa Mariamu. Kulingana na desturi za Kiyahudi, msichana aliyeposwa alikuwa mke wake aliyemposa ingawaje hawakukubaliwa kukutana kimwili mpaka sherehe ya arusi (Mal 2:14; Lk 2:3). Hivyo, ulikuwa ni uvunjaji wa agano, tena aibu kubwa, kwa msichana aliyeposwa kupata mimba nje ya ndoa. Kosa hili liliadhibiwa kwa msichana yule kupewa talaka na kuuawa kwa kupigwa mawe (Kum 22:23-24).

Kwenye njia panda

Sheria na tamaduni hizi zilimwacha kijana Yusufu kwenye njia panda alipotambua kwamba Mariamu ana mimba. Kwa upande mmoja, Yusufu alikuwa na haki ya kumshitaki Mariamu kwa wazee ili kumpa talaka mara moja. Kufanya hivyo

kungemfanya Mariamu kupata adhabu iliyostahili. Hivyo, angekuwa ametenda sawa na sheria za Mungu na kujiondoa kwenye lawama.

Lakini, ingawa ni ushuhuda mzuri kutenda haki, ni ushuhuda mzuri zaidi kutenda hiyo haki kwa njia sahihi. Haki ya sheria ilidai Yusufu kumpa Mariamu

talaka na kumwacha apambane na aibu na adhabu ya kuvunja agano la ndoa. Ndivyo

Yusufu alivyotazamiwa kufanya. Lakini kumbe, licha ya hisia nzito za kusalitiwa na mwenzake,Yusufu aliazimu kumwacha

Mariamu kwa siri (Mt 1:19). Kwa nini?

Sawa na sherehe ya uchumba ambapo familia zote mbili zilihusika, pia talaka

ilitolewa hadharani, sawa na adhabu ya kupigwa mawe. Hivyo, kwa kumpa talaka, Yusufu angekuwa amejiweka kuwa mshitaki mkuu wa Mariamu. Lakini Yusufu aliazimu kumwacha Mariamu bila kuchochea au kuchangia aibu au adhabu ya mwenzake kwa njia yoyote ile. Huku akizingatia hali na hisia za Mariamu pia, Yusufu aliazimu kumwacha Mariamu, lakini kwa njia iliyojaa upendo na neema - yaani, kwa siri.

Lingine tunalojifunza kutoka kwa

Yusufu ni kwamba anaishi maisha ya ushuhuda kama mtu aliye tayari kusikia, kuitikia na kumtii Mungu anaposema. Sidhani ni ndoto tu iliyomfanya Yusufu kubadili azimio lake la kumwacha Mariamu. Maana, zaidi ya ndoto, tunaona

uitikiaji na utayari wa kumtii Mungu ambao ni nadra tunapojipata kwenye

hali gumu kama ya Yusufu. Huu ni utii unaopuuza kufedheheshwa na watu ili tuenende anavyoongoza Mungu. Ni utii

unaotokana na kuamini kwamba Mungu

atashughulikia hata yale yaliyofichika

kwangu, kwa maana anayaona yote na anayaweza yote.

Ndiyo maisha ya kumtii Kristo Na mwisho, kuishi maisha ya ushuhuda kunajumuisha kutiisha hali zetu kwa

ajili ya Kristo. Yusufu hakuhitaji kibali zaidi kutoka kwa mwingine awaye yote baada ya Mungu mwenyewe kumwambia, “Usihofu kumchukua Mariamu mkeo” (Mt 1:20). Tena, kwa kuheshimu kazi ya Roho wa Mungu kwa Mariamu, na akijua kwamba mtoto alitabiriwa kuzaliwa na bikira, Yusufu hakumjua Mariamu mpaka alipozaliwa Yesu (Mt 1:25).

Bila shaka kijana Yusufu alikuwa mwanamume sawa kimaumbile, yaani alikuwa na hisia zote zinazoambatana na mume

aliyeoa kihalali. Kwa mtazamo huu, pengine ingekuwa heri kwake kumwacha Mariamu kwa wazazi wake hadi atakapojifungua mtoto Yesu. Lakini ni ushuhuda wa kipekee kwamba alimchukua, akawa mke wake wa halali sawa na neno la Mungu, akaishi naye kwenye nyumba moja akimpenda na kumtunza, na bado akajizuia kumjua kimwili hadi mtoto Yesu alipozaliwa.

Kuishi maisha ya ushuhuda ni kutiisha kila hali ya mwili na nafsi hata ku-

mtii Kristo, kama Yusufu. Mtu anayeishi maisha ya ushuhuda, ni huyu anayeweza kuteka nyara na kutiisha kila fikra mbaya (2 Kor 10:5), tamaa za mwili (1 Kor 9:26), na kuutia ulimi wake lijamu kwa ajili ya Kristo (Yak 3:8).

Yanawezaje maisha hayo?

Kwa nguvu zetu, au bidii tu ya utii wa sheria, hatutaweza kuishi maisha ya ushuhuda. Lakini, ninatiwa moyo kwa kujua kwamba wanaoitwa kuishi maisha ya ushuhuda sio malaika bali watu wa kawaida kama Yusufu, watu kama mimi na wewe. Tunachohitaji ni Yesu Kristo ndani yetu. Ndiye anayetufanya kuchukia uovu, na kuwa tayari kumtii Mungu anaposema nasi. Kwa kweli, Kristo akiwa upande wetu, sisi ni washindi katika yeye atakayetutia nguvu na kutuwezesha kuishi maisha ya ushuhuda (Rum 8:37).

9 8 RIZIKI TOLEO 1, 2023 RIZIKI TOLEO 1, 2023 WATU WA BIBLIA WATU WA BIBLIA
Mch. Gideon Mumo Picha: freeimages.com

Upendo wa familia ulinivuta kwa Yesu

maisha yangu. Ni kweli nilienda kanisani mara moja moja sana, lakini kwa mazoea tu kwamba kila Jumapili ni muhimu

kwenda kanisani. Siku hizo za ibada nilisoma Biblia, lakini hata sikuelewa vifungu vingi nilivyosoma. Lakini kupitia familia

hii ambayo ina ibada kila jioni, nimepata

kumjua Yesu na nimempokea kama Bwana na Mwokozi wangu.

Nilipofika kwa mara ya kwanza nyumbani kwao, nilivutiwa sana kuona

watoto wadogo kwenye familia hii ndio wanaoongoza ibada ya jioni. Jambo hili

lilikuwa geni kwangu. Nakumbuka siku ya pili mtoto mdogo aliongoza sala ya

kutumia mwongozo wa neno la kila siku. Nilimsikiliza kwa makini sana, maana na mimi nilikuwa na shauku ya kuwa kama wadogo zangu pale nyumbani kwa bosi wangu. Siku ile niliyofundishwa, sikuongoza ibada mimi, bali aliongoza mwingine, na mama akaniambia, “Fuatilia na kujifunza kwa umakini sana, kesho ni zamu yako.”

Kwa mara ya kwanza nilifika hapa Dar es Salaam miaka mitano iliyopita nikitokea kijijini kwetu Mugumu, Mara. Kule kijijini nilisoma na kuishia darasa la tano. Hali ya wazazi wangu haikuruhusu niendelee na masomo, hivyo nililazimika kuacha shule, na kuingia katika kazi ya kuchunga mifugo ya wazazi wangu.

Maisha yetu ya kule kijijini yalikuwa magumu, maana kuna kipindi hatukuweza kupata mahitaji yetu kama familia. Hata hivyo ninamshukuru Mungu, kwani Baba na Mama walijitahidi sana kuhakikisha kile kidogo wanachopata kinatusaidia kwa wakati huo.

Maisha ya kule kijijini kwetu yaliendelea kuwa magumu kwetu na baba yangu

alimwomba mjomba wangu anitafutie kazi yoyote mjini ili nipate fedha hata kidogo ya kuwasaidia wazazi wangu. Kweli, mjomba alikubali. Alinichukua na kuni-

peleka kwa rafiki yake ambaye alikuwa na mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo maeneo ya Kibaha. Nilipewa kazi ya kuchunga mifugo hii, na kwa kweli sikuona kama jambo gumu, kwa maana ni kazi niliyokuwa nimeizoea tangu kijijini.

Kilichobadilisha maisha yangu

Familia niliyokuwa naishi nayo walinipenda sana. Nilijiona kama sehemu ya familia. Na jambo kubwa lililonigusa na kubadilisha maisha yangu ni utaratibu wao mzuri wa kuwa na ibada kila siku

jioni. Hili lilikuwa jambo geni kwangu.

Kule kijijini nilizoea kwenda kanisani tu siku ya Jumapili, tena mara moja moja sana. Lakini kwa familia hii ibada ilikuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku kama ilivyo ratiba ya kuchunga mifugo.

Hapo kwanza sikuwa namfahamu

Kristo kama Bwana na Mwokozi wa

jioni. Alipomaliza kusoma neno na ufafanuzi kwenye kitabu cha neno la kila siku, aliniomba nifunge ibada kwa sala. Niliogopa na kutetemeka sana, maana sijazoea kufanya hivyo. Mama alinitia moyo kwa kusema, “Tafadhali Geofrey, omba hata kwa maneno machache tu. Mungu anasikia!”

Sitasahau kamwe sala niliyoomba jioni hiyo. Hivi ndivyo nilivyoomba, “Asante, Mungu, kwa kumlinda Baba na Mama kazini, na watoto shule na mimi. Wote tumerudi salama nyumbani. Tulinde tunapoenda kulala. Amen.”

Mama alifurahi sana na kunipongeza kuwa nimesali vizuri. Watoto pia wakaniambia, “Kaka Geofrey, umeomba vizuri.” Maneno haya yalinitia moyo, na nikawa natamani kila siku na mimi nijue jinsi ya kuendesha ibada ya jioni pale nyumbani.

Kuongoza ibada mara ya kwanza Siku moja jioni mama aliniita na kuanza kunifundisha namna ya kuendesha ibada

Kesho ilipofika nilikuwa na hamu sana jioni ifike. Wakati nilipokuwa ninakata majani ya mifungo, nilijikuta ninaimba tu nyimbo za ibada. Shauku hii iliendelea hadi jioni ile ambayo nilipewa zamu kwa mara ya kwanza kuongoza ibada. Halikuwa jambo gumu, maana nilikuwa ninatumia mwongozo wa neno la kila siku.

Kwa kweli ibada hizi za jioni zimenijenga sana kiroho na kiimani tofauti na nilivyokuwa nilipokuja kutoka Musoma. Nimejifunza mengi kupitia majadiliano wakati wa ibada, na pia siku hizi ikipita Jumapili ambayo kwa bahati mbaya sijaenda kanisani, najisikia deni moyoni mwangu, na tena naona ni kama wiki bado haijaisha.

Ukiniuliza leo ni nini kilichonibadilisha na kuwa Mkristo anayempenda Mungu, jibu langu nitakuambia, “Ni upendo wa familia ya bosi wangu ambaye namsaidia kazi ya kuangalia mifugo yake.” Familia hii imekuwa familia bora sana, kwa maana licha ya kunipa mshahara, pia wanawasaidia wazazi wangu kule kijijini. Upendo wao kwangu ndio ulionivuta nimwone Yesu ndani yao na kutamani nami kuwa naye vilevile.

11 10 RIZIKI TOLEO 1, 2023 RIZIKI TOLEO 1, 2023 USHUHUDA USHUHUDA
Senteu Marwa Picha: freeimages.com

Kuitangaza mauti ya Bwana hata ajapo

Mchango kwa maandalizi ya kuhubiri juu ya 1 Wakorintho 11:26

mbayo kwayo

Yesu alianzisha chakula chake (1 Kor 11:23-25; ling. Mt 26:2629).

angalie mimi ninayeshiriki, bali huwavuta

wote wanaojisikia wenye dhambi waje

kwa Yesu.

Kushuhudia kuja kwa Yesu

Yesu alipoanzisha chakula chake kwenye

sherehe ya Pasaka ya Kiyahudi, alifafanua

maana yake akisema, Nimetamani sana

kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya

Mpangilio wa mahubiri

Utangulizi:

Maisha yetu hushuhudia nini? Yesu alisema, Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya (Lk 24:48). Kufafanua mambo hayo kwa ufupi.

Mada kuu:

Ushuhuda ni jibu la imani. Twamshuhudia Mwokozi na Bwana wetu kwa maneno. Lakini twamshuhudia pia kwa matendo yetu, na katika Biblia kuna tendo fulani lililotajwa moja kwa moja kama

ushuhuda juu ya Yesu:

Kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya

Bwana hata ajapo.

Neno hilo “kutangaza” linamaanisha

kwamba tunaposherehekea chakula cha

Bwana, tunahubiri na kusifu kwa uwazi

mambo mawili kuhusu Yesu: Alikufa kwa ajili yetu, na atakuja tena duniani.

Kushuhudia mauti ya Bwana

Habari ya kuitangaza mauti ya Yesu

ina-fuata mara baada ya maneno yale a-

Mwili wa Yesu ulitolewa ili kuzichukua dhambi zetu juu ya msalaba, ambapo damu yake ilimwagika ili kutuletea ondoleo la dhambi zetu. Tunapopokea mwili huo na damu hiyo kwenye meza ya Bwana, siyo tu kwamba sisi wenyewe tunakumbushwa habari hiyo njema, tunaihubiri pia. Tendo laweza kushuhudia zaidi ya maneno mengi. Ndivyo ilivyo na tendo la kupokea chakula cha Yesu. Ni ushuhuda hasa, tena ushuhuda maradufu.

Maana kwa kule kushiriki kwetu tu, twawaambia wengine jinsi hali yetu ya kweli ilivyo. Kwa kupiga magoti chakulani kwake, au tendo linginelo la unyenyekevu, twakiri tu wenye dhambi wasiojiweza.

Wakati huo huo twawaambia watu wote kwamba hapo chakulani tunakutana na Yesu, naye ndiye Mwokozi hai anayewapokea wenye dhambi na kutupa msamaha na uzima.

Ushuhuda huo hauwavuti watu wani-

kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa

katika ufalme wa Mungu (Lk 22:15-16).

Hivyo aliwapa wanafunzi wake tumaini

kwamba watakuwa pamoja naye tena

kwenye uzima wa milele (Yn 6:54).

Wakati huu tunaposhiriki chakula cha

Bwana, Yesu ni mwenye karamu. Kwa kukutana naye hapo mezani, tunatiwa tumaini kwamba Yesu atakuja tena kimwili hapa duniani. Tunakiri kwamba Mwokozi

na Bwana wetu yuko hai, na tunatangaza

kuja kwake mara ya pili.

Chakula cha Bwana ni kiungo kati ya kuzaliwa kwa Yesu kwenye unyonge

na kuja kwake kwa nguvu na utukufu mwingi.

Maana yake kwao wanaomfuata Yesu ni kwamba wako safarini. Chakula cha Bwana ni mlo wa safari. Kama wana wa Israeli walivyokula Pasaka wakiwa tayari kuanza safari ya kwenda nchi ya ahadi, meza ya Bwana ni mahali wanapojengwa kiroho Wakristo walioko njiani kwenda alipo Yesu.

Pamoja na kushuhudia kuja kwa Yesu, tunajishuhudia kuwa tu wageni hapa duniani. Kama raia wa Ufalme wa Mungu tuko safarini kwenda kwa nchi ya nyumbani.

Ushuhuda wetu tunaposhirikiana chakula cha Bwana

1) Kwenye meza ya Bwana twamshuhudia Mwokozi wetu kwamba alikufa kwa ajili ya dhambi zetu ili kutupatanisha na Mungu, tena sisi kwa sisi. Wakati uohuo tunajishuhudia wenyewe kwamba tu wenye dhambi tunaohitaji na kupokea ondoleo la dhambi hapo mezani kwa Yesu. Anatufanya kuwa watu wamoja wa Mungu kwa kutushirikisha mwili na damu yake.

2) Kwenye meza ya Bwana twamshuhudia Bwana wetu kwamba yu hai na kutushirikisha ushindi wake juu ya mauti. Tunatangaza ahadi yake kwamba atakuja tena kutukaribisha kwake, ili alipo yeye, nasi tuwepo. Wakati uohuo tunajishuhudia wenyewe kwamba tu wageni na wasafiri hapa duniani tunaotazamia mbingu mpya na dunia mpya ambayo haki yakaa ndani yake.

Hitimisho:

Ushuhuda wetu wa kikristo hasa ndio kumshuhudia Kristo Yesu, Mwokozi na Bwana wetu. Siri ya ushuhuda huo imebainika katika Rum 1:16! Moyo na ujasiri wa kufanya hivyo tunatiwa hapo chakulani kwa Yesu tunapoonja Bwana wetu alivyo mwema.

13 12 RIZIKI TOLEO 1, 2023 RIZIKI TOLEO 1, 2023 IHUBIRI INJILI IHUBIRI INJILI
Picha: www.pixabay.com Mch. Philip Bach-Svendsen

Ibada huanzia nyumbani

“Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako” (Kum 6:4-9).

Mungu ndiye Mwanzilishi

Watoto ni zawadi kutoka Mungu. Hivi ndivyo ilivyokuwa tangu mwanzo. Katika

Agano la Kale wana wa Israeli walichukulia kitendo cha kupata mtoto kama baraka ya Mungu anayoweza kumpa mwanadamu. Mtazamo huu unatiwa nguvu na mtunga zaburi anaposema, “Tazama, wana ndio urithi wa Bwana, uzao wa tumbo ni thawabu’’ (Zaburi 127:3).

Baada ya wana wa Israeli kukaa jangwani kwa miaka 40 kwa sababu ya kutokumwamini Mungu, kwa mara nyingine tena Musa aliwakusanya na kuwakumbusha maneno na matendo ya Mungu ili kuwaandaa kwa upya kuingia katika nchi ya ahadi. Jambo kubwa ambalo walipaswa kujifunza wakati huu, lilikuwa ni ahadi zake Mungu ili wamtegemee na wawe utii wa imani.

Ili waweze kuingia na kuishi katika nchi ya ahadi kama Mungu atakavyo, walihitaji Mungu kuwapa maelekezo ya vitendo. Walihitaji kuyasikiliza hayo kwa

makini ili wawezeshwe kuwa waaminifu katika kuishi jinsi inavyompendeza Mungu.

Imani nyumbani

Mafungu ya Kumbukumbu la Torati 6:49 yanaangukia katika sehemu kuu mbili. Mosi, kuna ukweli mkubwa ambao mwanadamu anaweza kugundua maishani, yaani ukuu wa Mungu. Na pili, ukweli kuhusu uhusiano wa mwanadamu na Mungu. Kanuni kuu ya kumcha Mungu ni upendo. Na si kumpendapenda tu, bali kumpenda “kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote” (mst. 5).

Hii ilikuwa ndiyo amri kuu na ya kwanza kwa Israeli, na katika mst. 7 tunaona kwamba wa kwanza katika kushirikisha amri hii kwa vizazi vijavyo ndio wazazi. Wana wa Israeli walipewa maelekezo na Mungu ya kuwafundisha watoto wao kuwa na uhusiano na Mungu na kumpenda, si kwa kwenda sehemu za kuabudia tu, bali waliambiwa wafanye hivyo kuanzia nyumbani kwao, wanapotoka na kuingia, na hata wanapolala.

Ukuu wa amri hili unathibitishwa na Yesu akimjibu mwanasheria mmoja aliyemwuliza swali kuhusu kupata uzima wa milele. Hapo Yesu anainukuu hiyo kama amri ya kwanza akimwambia, ‘”Mpende

Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa nguvu zako zote” (Mt 22:38-39).

Katika kanisa la nyumbani kuna nafasi nzuri ya kufundishana juu ya kumpenda Mungu, tena kwa vitendo, maana kila mtu anajifunza kutoka kwa mwenzake.

Kwa nini nyumbani?

Nyumbani ni mahali ambapo watoto wanaanza

kujifunza tabia ya Mungu kwa kuangalia maisha ya wazazi wao. Tena ni mahali sahihi ambapo familia inaweza kukaa pamoja na kupata chakula, kuongea kwa pamoja na kujifunza kwa urahisi. Katika

Mithali 4:3-4 mwandishi

anatupa umuhimu wa wazazi kuwafundisha watoto

imani ya Mungu kuanzia

nyumbani akisema, “Nalikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu. Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu;

shika amri zangu ukaishi.”

Ni matamanio ya Mungu kuwa watoto wafundishwe kumjua Yeye na kushika neno lake tangu wakiwa wadogo.

Mahali sahihi pa kuanzia ni nyumbani ambapo watoto na wazazi wanaweza kutumia muda kila siku kukaa pamoja na

mwanadamu. Mfano mzuri ni jinsi Paulo anavyokumbuka hali ya familia ya Timotheo: “Niikiumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo” (2 Tim 1:5).

kufundishana anayosema Mungu kwa

kuyanena katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo na uondokapo“ (mst. 7b). Maana ya mstari huu ni kwamba wakati wa ibada pale nyumbani watoto

waambiwe kweli ya Mungu inayohusiana na maisha yao ya kila siku.

Wafundishwe kutoka kwenye Biblia, lakini pia maisha ya wazazi wao yawe

kielelezo na yanayomwakilisha Mungu ili iwe rahisi kwa watoto kujifunza na kuelewa kuhusu uhusiano wa Mungu na

Nyumba yenye ibada huwa na tofauti kubwa na ile ambayo haina ibada, maana kwenye ibada Mungu yupo na kuwafundisha wote wanaoshiriki jinsi ya kukaa pamoja kwa umoja na upendo wa kweli. Yoshua anasisitiza umuhimu wa ibada kuanzia nyumbani anaposema, “Mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana’’ (Yos 24:15). Huwezi kumtumikia Bwana pamoja na nyumba yako kama hakuna ibada wala umoja ndani ya nyumba.

15 14 RIZIKI TOLEO 1, 2023 KANISA
RIZIKI
1, 2023
LA NYUMBANI
TOLEO
KANISA LA NYUMBANI James Sabuni Picha: www.pixabay.com

Mwongozo mpya wa mahubiri!

Nadharia na vitendo vinaendana

katika mwongozo huu wa mahubiri ya sheria na injili.

Mwandishi anakusaidia kuelewa

mawazo ya wataalamu, na kukukaribisha kwenye chumba chake

anapoandaa mahubiri ili uweze

kuona jinsi anavyofanya na kuhojiana naye kuhusiana na

mbinu zake za kuhubiri. Anatoa pia mifano ya mahubiri yake ili uweze kujifunza kama msikiaji. Ujumbe

wake ni wazi:

Sheria husema, “Unamhitaji

Kristo!” na Injili hutangaza, “Kristo yuko hivi naye ni wako!”

Mungu abomoapo na kujenga kitakutia hamu ya kwenda mimbarini

kuhubiri Injili ya Yesu Kristo.

Kitabu kinapatikana Soma Biblia

RIZIKI TOLEO 1, 2023 SOMA BIBLIA 0759 544 917 S.L.P. 2696, Arusha editor.somabiblia@gmail.com www.somabiblia.or.tz Soma RIZIKI “online” www.issuu.com/riziki
Issuu converts static files into: digital portfolios, online yearbooks, online catalogs, digital photo albums and more. Sign up and create your flipbook.