
3 minute read
Mjue mwanasoka wa KNHFC
Na Luke Kung’u
Kocha George Makambi
Advertisement
Bw. Makambi ndiye kocha wa timu ya mpira wa miguu ya KNHFC na hujivunia kuwa na tajriba pana tena ya hali ya juu kuhusu soka. Ndio kujua mengi kumhusu, tulimwalika kwa kikao atueleze kuhusu kipaji hiki chake.
Karibu Bw. Makambi.
Tungependa kwanza utueleze kwa kifupi wewe ni nani kikazi, kifamilia na hata ukipenda historia yako ya ujana na umalizie kwa upendo wako wa mpira wa miguu.
Kwa majina naitwa George Makambi kocha mkuu wat imu ya kitaifa KNHFC. Bali na kuwa kocha aliyehitimu na kujipatia leseni ya CAF C ambayo nilihitimu mwaka wa elfu mbili na kumi na moja (2011). Kikazi nafanya kwenye kitengo cha usimamizi wa raslimali watu ama ukipenda Human Resource Division kama afisa mkuu wa rasilimali watu (Senior Human Resource Officer) hadi wa leo.
Historia yangu ya kupenda soka ilianzia nikiwa na umri wa miaka tano ambapo nilikuwa natumia muda mwingi kutazama mechi kadhaa kwa runinga sanasana kipindi cha ‘Football made in Germany’ pamoja na ‘FA Cup’.
Ni lini na ni matukio gani yalikufanya ukapenda mpira wa miguu kuliko michezo mingine mpaka ukawa kocha?
Nikiwa kijana mdogo, pamoja na vijana wengine kijijini, tulikuwa tukijiundia mipira tukitumia nyuzi na matambara. Ilikuwa rahisi kuunda na ilipoumbuka tuliweza kuishona na kuendelea kucheza. Enzi hizo mpira wa miguu ulikuwa kigezo kikuu kwa vijana.
Ni mechi gani chini ya uangalizi wako mlifanya vyema na ni gani mlifanya vibaya?
Kwa uongozi wangu, timu ya vijana chipukizi wa chini ya miaka kumi na nne iliyojulikana kama KNHYouth, ilijishindia kombe la Afrika mashariki mwaka wa elfu mbili kumi na tano (2015).
Hawa wachezaji wa timu ya KNHFC hutumia njia gani kuwachunja na kutofautisha wanaofaa kujiunga?
Hili ni swali mboga kabisa. Uwanja wa mpira wa miguu huwa umegawanywa kwa sehemu nne: golikipa, ulinzi, katikati na ushambulizi. Wachezaji hujipambania kwa kadri ya uwezo wao katika vijisehemu hizo nne. Kwa kuangalia uchezaji wao ninaweza kubaini aliye bora na kumchagua.
Kwa ujumla umechezesha mechi ngapi tangu uwe kocha?
Kwa ujumla nimeweza kusimamia mechi elfu tatu mia tano (3,500) kama kocha.
Kama kocha, ilhali wewe ni mfanyi kazi, ni nini unaweza sema ni changamoto kubwa inayoathiri utenda kazi?
Kuna changamoto kibao. Hatuna uwanja mzuri wa kufanyia mazoezi na hata vifaa vya kufanyia mazoezi hayo. Imekuwa ngumu kuisitiri timu kifedha kwa sababu wachezaji wengi wa KNHFC sio waajiriwa wa hospitali kuu ya rufaa ya Kenyatta, hawa vijana hawana ajira ila ningeomba ikiwezekana wapewe nafasi ya kikazi hospitalini.
Umewahi pata zawadi yoyote kama kocha ama mchezaji?
Zawadi nazo nimejinyakulia nyingi. Nakumbuka kama ni jana tu tulipojishindia kombe la chipukizi
wasiozidi umri wa miaka kumi na mbili na kumi na nne katika kombe la dunia la chipukizi Gothenburg nchini Uswizi mwaka wa elfu mbili na saba (2007).
La ziada?
Tupatane uwanjani. Shukran kwa muda wako.

Bw. George Makambi, Afisa mkuu wa rasilimali watu
PICHA | COURTESY