waandishi ebook 1687869185.8334353

Page 1

Kisa cha Panzi na Kunguru

Mwamwingila G.P

Mtalimbo Books

i

Kimepigwa chapa na kampuni ya

African Market Agencies (T) Ltd mwaka 2022

Haki zotezimehifadhiwa

Copyright©Goima Mwamwingila 2020

ISBN 978-9976-5714-6-2

Chapa ya kwanza2020

Chapa ya pili 2022

Kitabu hiki kinalindwa na haki miliki. Si ruhusa kukichapa tena ama kutumia sehemu ya maandiko yake ama mawazo yake kwa shughuli yoyote ya kibiashara bila makubaliano na ruhusa ya maandishi toka Mtalimbo Books.

Baruapepe: mtalimbobooks@gmail.com

Simu: +255 754 075 891, +255 657 532 334

Kitabu hiki ni kazi ya kubuni, majina ya sehemu na wahusika wote ni kazi ya Sanaa ya ubunifu, hivyo kufanana kwa watu

walio hai ama waliofariki kusihusishwe na kutafsiriwa katika

uhalisia kwa namna yoyote ile kwa kuwa mwandishi ameishi katika mazingira ya watu wa kawaida ama vitu vinaweza

kufanana na kazi yake ya sanaa kwa kiasi fulani.

iii

Tabaruku

Hadithi hii nimeitunga kama zawadi maalumu kwa

Watoto wa Afrika, wapate kutambua umuhimu wa utawala bora, kupendana, kuaminiana na

kushirikishana katika maamuzi yenye manufaa kwa

Mataifa yao na Bara zima la Afrika.

iv

DIBAJI

Afrika ni bara tajiri, tajiri kwamaana ya utajiri, iwe nimoyo wa wanaafrika wenyewe, ardhina rasilimali nyingine nyingi mno.Pamoja na yote hayo Afrika imeachwambali sana kwa maendeleo kuanzia siasampaka uchumi.Ukitambua hilo bado utakuwa na kazi ya kujiuliza ni kwa vipi tajiri akawamaskini na maskini akawa tajiri?

Kujibu ama kutegua kitendawili kunahitaji sana kuangalia ni wapi umesimama na wapiunaangalia, ikiwa umesimama kilimani unaangazabondeni ni dhahirihatamiti mirefu ikukinge bado utaweza kuona mbali lakini ikiwa utasimama bondeni na kukingwa hata na jabali la wastani tu ukiongeza na labda mwanga wa jua unaokumulika usoni basi ni aghalabu kuona yanayojiri kilimani.

Kisa cha mafahari wawili Panzi na Kunguru ni kielelezo tosha

kuwa Afrika ingali bondeni na inapambana kuangaza kilimani bila ya kukwepa majabali yanayozibamacho kupata nuru ili kufikia lengo la kuridhisha macho yake.

ShimeShime Afrika tuwabaini kunguru na hila zao.Kunguru wanaweza kuwa wambaliamahata jirani na ndugu wa damu ama rafiki wa kila leo.

HUSSEIN WAMAYWA

Mshindi wa tuzo ya fasihiya Kiswahili ya Mabati Cornel ya

Fasihi ya Kiafrikamwaka 2016

v

SHUKRANI

Kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa uwezo wa kufanya kazi hizi za utunzi kwa weledi mkuu.

Pili naishukuru familia yangu, marafiki na hasa watunzi wenzangu kwani changamoto wanazonipa ndio chachu ya uandishi wangu.

Mwisho mazingira na changamoto za bara la Afrika zimkuwa msukumo mkubwa wa kuandika kazi hii.

Mwisho japo sio kwa umuhimu ni watendaji wa ngazi

mbalimbali kuanzia Baraza la Kiswahili Taifa

(BAKITA), African Market Agenies (T) Ltd na Mtalimbo Books kwa kunisimamia mpaka kazi hii inafikiahatua ya kusomwa na jamii kusudiwa.

vi

Sehemu ya 1

Uadui wa Panzi na Kunguru

Hapo zamani za kale, palitokea Panzi na Kunguru, ambao walikuwa ni maadui wakubwa. Uadui wao

ulikuwa ni kwa sababu ya Kunguru kuwalaghai Panzi na kuwafanya waishi maisha ya tabu.

Hapo awali, Panzi walikuwa na elimu nzuri kuanzia

Shule za Awali mpaka Vyuo vikuu. Panzi waligundua

vitu kama; moto, hesabu, waliweza kujenga majengo

makubwa zaidi duniani, walikuwa na Serikali nzuri na

1

Miji mizuri. Si hayo tu, bali waliheshimiana wao kwa wao, walikuwa na urafiki wa kweli. Wote waliwatii

viongozi wao, hawakuwa na tamaa ya madaraka na walijituma kufanya kazi kwa bidii na waliishi kwa kushirikiana.

Panzi walikuwa wakulima hodari japo walitumia dhana

hafifu, walilima mazao mengi na kuyahifadhi kwenye maghala ya vyakula.

Panzi walikuwa na madini na vito vya thamani, kwa kuwa nchi yao ilibarikiwa kuwa na madini mengi ambayo hayakuwepo katika nchi ya Kunguru.

Japo Kunguru walikuwa na nguvu za kufanya kazi, nchi yao ilikuwa na miamba mingi pia ilikuwa na vipindi

virefu vya baridi kali, hali iliyowafanya Kunguru kutumia akili nyingi sana ili waweze kuishi kwa raha

mustarehe kama walivyoishi Panzi.

Kunguru hawakupenda kufanya kazi nzito, hivyo mara nyingi waliwarubuni Panzi kwa kuwatumia kama

wafanya kazi wao. Baada ya Panzi kuwatumikia

Kunguru kwa muda mrefu, Kunguru waliwauwa Panzi na kuwala.

2

Sehemu ya 2

Kikao cha Kunguru

Siku moja, kunguru mkuu aliitisha kikao na kunguru wote walihudhuria. Walikuwepo Kunguru wenye doa

jeupe, wanene, wembamba na weusi tii.

Kunguru mkuu akawaambia “ninyi nyote mnafahamu ya kuwa nchi yetu haina madini mengi kama ya nchi ya

Panzi, hatuna hali ya hewa nzuri, kipindi kirefu ni baridi kali mpaka barafu, tunakosa muda wa kuandaa chakula kwa wingi na ikifika msimu wa hali ya hewa mbaya vifo vinatuandama.

Kunguru alivuta pumsi ndani na kuitoa nje akipumua kidogo kisha aliendela. “Tunahitaji kufikiri vizuri ili kubaki hai na wenye afya. Tutafanyeje ili na sisi tuwe na chakula na tuache kula jalalani?’’

Kunguru walitoa maoni yao, na kupokelewa kwa heshima na usawa. Wengine wakasema walime, Wengine wakasema wakawinde na kukausha nyama kisha waweke kwenye ghala.

3

Kunguru mmoja mwenye akili nyingi akasema ‘’hamna haja ya kulima wala kuwinda maporini kwa wanyama

wakali, ila tutumie akili ya kuzaliwa. “Taifa linalofikiri kwa kina ndio Taifa litakaloongoza dunia”

Kunguru mkuu akauliza “akili hiyo ni ipi, ya kutufanya

tuwazidi Panzi? Maana wao wana kila kitu”.

Basi Kunguru mwenye akili nyingi akawaambia wenzake. “Tazama nchi ya Panzi ina mali nyingi, ardhi

nzuri na utawala mzuri na wananchi wake ni watii kwa

viongozi wao, lakini kuna jambo moja kubwa naliona miongoni mwao”

“Jambo gani hilo unaloliona na unadhani linaweza kutusaidia?” Kunguru mkuu alihoji.

Kunguru mwenye akili nyingi akasema tena “Panzi wanakasoro moja tu, kasoro hiyo ni Ubinafsi wa viongozi wao, viongozi wao wanapenda sana

kujipendelea wao na familia zao, pia wanapenda sana kusifiwa.

Wapo radhi hata kuwauza Panzi wenzao ikiwa

tutawaahidi zawadi ndogondogo tena zisizo na thamani, tena wanaamini kila jambo unalowaambia bila hata kuchunguza kwa umakini”

4

Kunguru mkuu akasema, “Kama unayosema ni kweli basi tutume watu wetu waende kuwadanganya, ikiwa wataamini uongo wetu basi tutawachonganisha wao kwa wao na ikiwa watagombana basi sisi hakuna haja ya kulima maana wao watapigana na kufa halafu sisi tutapata chakula na mali kwa urahisi” Kunguru wote waliafiki.

5
6

Sehemu ya 3

Uongo wa Kunguru

Mkuu wa Kunguru akatuma wapelelezi wake na ujumbe mzito, nao wakaenda mpaka kwa Panzi mkuu, wakafanya kikao nae, kama walivyoafikiana kule katika kikao chao na mipango yao.

7

Kunguru wakamwambia Panzi mkuu, “Panzi msaidizi wako anatuuzia chakula na madini kwa bei ndogo

kuliko unayotuuzia wewe” Panzi mkuu akaendelea kuwasikiliza Kunguru.

Kunguru wakaendelea kusema, “msaidizi wako atakuwa tajiri mkubwa tena ana mipango ya kuhama na kuja

kuishi nasi Kunguru kwenye miti mirefu, yeye na watu wake”.

Panzi mkuu alianza kukasirika, akawauliza wale Kunguru “Je, ni kweli Panzi msaidizi ananisaliti?”

Kunguru wakamwambia “Ni kweli, sasa fikiri Panzi wengine wasioweza kuruka juu sana, wataishi vipi?”

8

Uongo huu ulimfanya Panzi mkuu akasirike sana.

Alipojaribu kumuita Panzi msaidizi, hakuwepo basi

akaamini kuwa tayari ametoroka. Panzi mkuu

akaamrisha vita dhidi ya kundi lote la Panzi msaidizi.

Panzi msaidizi na kundi lake walikuwa wameenda

kuchimba madini kwa ajili ya kwenda kuuza ili

wapeleke pesa kwa Panzi mkuu, lakini Panzi mkuu

9

alipowaona na madini aliamini Panzi msaidizi alikuwa anatoroka namadini.

Panzi mkuu hakuwa mvumilivu, wala hakutaka hata

kuongea na Panzi msaidizi ili kujua ukweli juu ya taarifa alizopewa na Kunguru.

10

Sehemu ya 4

Uwanja wa Mapambano

Jeshi la Panzi mkuu liliuvamia msafara wa Panzi msaidizi na kuanza kuwapiga.

Baada ya muda mfupi, mapigano ya Panzi yalipamba moto, wakarushiana mishale, mabomu na risasi.

Wakauana wao kwao na kusahau kuwa wao ni ndugu.

Kunguru walipoona mapigano yamekolea kati ya Panzi, Kunguru wakajigawa makundimakundi, kundi moja

11

likampelekea silaha Panzi mkuu na kundi lake, kundi jingine likapeleka silaha kwa Panzi msaidizi na wafuasi wake, vita ikawa kali zaidi, kundi jingine likaandika hadithi kuwa “Panzi sio ndugu tena na hawapendani”, kisha likasambaza dunia nzima.

Kwa kuwa Panzi walikuwa hawana akili walipokea silaha na mapigano yakawa makali zaidi. Panzi walipigana sana na wengi walikufa.

Kunguru walikuwa wanapita na kukusanya mizoga ya

Panzi. Kwa kuwa Panzi waliathirika sana kwa vita, hawakuweza tena kuendesha mashamba yao wala kulinda madini na rasilimali zao.

Mpaka leo Panzi wamebaki masikini, wanapigana vita wao kwa wao kila kukicha. Panzi hawana tena umoja, hawana mashamba makubwa, wala hawajengi majengo makubwa ya kudumu.

Hawana ulinzi wa mali zao kama vile wanyama na madini. Panzi wanalipa madeni ya silaha walizochukuwa kwa Kunguru kwa ajili ya kuwapiga na kuwaua Panzi wenzao.

12

Panzi wamejenga majumba makubwa ya kuhifadhi

silaha za gharama kubwa wanazonunua kwa Kunguru

badala ya kujenga maghala ya chakula kama

ilivyokuwa hapo zamani.

Siku hizi Panzi wana ombaomba chakula kwa Kunguru, akishiba ndio anawatupia Panzi na mara nyingine

Kunguru wanawauzia Panzi vyakula na ikiwa

watapandisha bei, basi Panzi wengi watakufa kwa njaa.

Mkuu wa Kunguru alifurahi sana akasema kweli “Vita vya Panzi, furaha ya Kunguru”

13
14

Sehemu ya 5

Majuto ya Panzi

Baada ya Panzi wengi sana kuuawa, vita ilisimama na Panzi wakaamua kwenda vijijini ili wakazaane waongezeke halafu warudi vitani.

Siku moja Panzi mkuu aliokota kipande cha karatasi chenye hadithi iliyoelezea kuwa Panzi sio ndugu.

Panzi mkuu alitafakari sana na kugundua kuwa mwandishi alikuwa na hila juu ya undugu wa Panzi.

Panzi mkuu aliumia sana kusoma hadithi za vita vya

Panzi kwamba “Panzi sio ndugu na wala hawapendani” kama ambavyo mwandishi Kunguru.

Kunguru aliandika kipindi cha vita vya Panzi. Panzi alibaini ya kuwa huu ulikuwa ujanja wa Kunguru, ili vizazi vya Panzi viendelee kuwa na chuki baina yao.

Panzi mkuu aliamua kuandika kitabu chake chenye

kuelezea ukweli kuwa Panzi wote ni wamoja na

wanatakiwa wakumbushwe kuwa wao ni ndugu, ila walichonganishwa na Kunguru.

15

Panzi mkuu aliamini kuwa, Panzi wakitambua na kukumbuka vema undugu wao wataungana tena na watakuwa Taifa kubwa zaidi ya taifa la Kunguru.

Wakati akiendelea kutafakari jinsi atakavyoandika na kukisambaza kitabu chenye ukweli kuhusu Kisa cha Panzi na Kunguru, Kuku alitokea na kumkimbiza Panzi ili amle.

Panzi akakimbia na kuangusha kitabu chake. Mpaka leo Panzi wengine hawajagundua ukweli kuwa Kunguru ndiye mchonganishi, pia ubinafsi wa viongozi wao ndio uliwafanya Panzi kupigana mpaka kuuana na hiyo kuwa furaha ya Kunguru.

MWISHO

16
Issuu converts static files into: digital portfolios, online yearbooks, online catalogs, digital photo albums and more. Sign up and create your flipbook.